21 December 2011

Maafa Dar

*Mvua kubwa yasababisha mafuriko, upotevu wa mali
*Waishio mabondeni wakosa makazi, vifo vyaripotiwa
*JWTZ, Polisi watumia helikopta zao kuokoa wananchi
*Serikali kutumia polisi kuhamisha wananchi kinguvu

Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, jana walikubwa na mafuriko, baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha baadhi ya nyumba kujaa maji na watu kukosa makazi kama inavyoonesha katika picha hizi.
Na Flora Amon

MVUA kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana hadi asubuhi katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam, imesababisha vifo, uharibifu wa mali na
mafuriko katika mitaa mbalimbali.

Barabara nyingi zilishindwa kupitika kirahisi kutokana na ubovu wa miundombinu ya kupitisha maji hivyo kusababisha uharibifu wa vyombo vya usafiri hususan magari na pikipiki ambazo nyingi zilitumbukia katika mifereji iliyoziba.

Wakazi wa mabondeni nao wamepata hasara kubwa ya kupoteza mali na kukosa makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.

Kutokana na maafa hayo, Mkuu wa Mkoa huo Bw.Meck Sadick alisema Serikali italazimika kutumia jeshi la polisi ili kuhamasisha wananchi waishio mabondeni kuhama maeneo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kutembelea maeneo mbalimbali yaliyoathirika na mvua hizo, Bw.Sadick alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), ilitoa tahadhari kwa wananchi waishio mabondeni kuhama maeneo hayo lakini ushauri huo umepuuzwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, helikopta inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na ile ya jeshi la polisi, jana ilifanya kazi kubwa ya kuokoa wananchi ili kunusuru maisha yao.

“Wananchi waishio mabondeni baadhi yao ni jeuri, Serikali imekuwa akitoa agizo la kuwataka wahame mabondeni lakini hawataki, wengine wanaendelea kujenga nyumba za makazi siku hadi siku, sasa tutatumia nguvu kuwahamisha kwani wengi wao wamejenga katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria,” alisema.

Bw.Sadick aliwataka wakazi wa Dar es Salaam, waache kuharibu mazingira kwa kutupa taka katika mitaro ambayo mingi imeziba kutokana na kujaa taka.

Aliongeza kuwa, umefika wakati wa kila Mtanzania kuishi kwa kufuata sheria, kujenga sehemu zilizopimwa na kupewa kibali ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza.

Alisema Serikali iliwahi kuwapa viwanja wakazi wa Jangwani ambao walipaswa kuhamia Yombo Dovya, Wazo Hill nyuma ya Kiwanda cha Saruji na Mbweni JKT pamoja na kupewa vifaa vya ujenzi kama mbao na mabati.

Aliongeza kuwa, pia Serikali iliahidi kuwapa usafiri wa kuhamisha matofali yao lakini waliuza viwanja hivyo na kuendelea kuishi Jangwani.

“Mafuriko yaliyotokea jana, yameleta maafa makubwa katika Wilaya ya Kinondoni, baadhi ya madaraja yameharibika hususan katika Bonde la Tabata, Kigogo, Mto Ng'ombe ambao unaunganisha Sinza na Tandale, Magomeni, Kwa Mtogole na Daraja la Msewe,” alisema Bw.Sadick.

Majira lilishuhudia baadhi ya maeneo yakiwa yamezungukwa na maji pamoja na wakazi wa Jangwani kulalamika kuwa, wamepoteza mali zao ambazo zimesombwa na maji yakiwemo magodoro na fedha taslimu za kujikimu.

Wakati huo huo, watu watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti yaliyotokana na mvua hizo likiwemo la mwanaume mmoja Bw.Ibrahimu Lutuma (65), mkazi wa Ubungo Msewe, kusombwa na maji baada ya kuangukiwa na ukuta.

Akizungumza na Majira, mpangaji katika nyumba iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu, Bi.Agnes Pitter (25), alisema asubuhi saa 12, maji yalianza kuingia ndani ya nyumba yao hivyo alilazimika kwenda kumuita marehemu ili ajionee hali hiyo.

“Marehemu aliamka na kwenda nje, wakati anarudi ndani aliangukiwa na ukuta wa chumba kimoja ambacho ni fremu ya biashara hivyo akawa anaelea kwenye maji ambayo yalimpeleka hadi katika Mto Ng'ombe ambao tupo nao jirani,” alisema.

Alisema wakati marehemu akiwa anaelea, alipiga kelele ndipo kijana mmoja ambaye hamfahamu alijaribu kumuokoa marehemu lakini alishindwa kwani maji yalikuwa yanaenda kwa kasi ambapo baadaye alisikia mwili wa marehemu umepatika katika mto huo eneo la Urafiki.

Mvua hiyo pia ilisababisha kifo cha Bi.Gati Mseti (39), mkazi wa Ukonga ambaye alifariki katika eneo la Shimo la Udongo baada ya kupigwa na radi wakati mtoto Maganga Said anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 10-15, alifariki dunia baada ya kushika waya wa umeme ambao uliangushwa na mvua hizo.

Maafa mengine yametokea Mbezi Temboni, eneo la Chazamani ambapo daraja lililojengwa na wananchi kwa kushirikiana na Mbunge wa Ubungo, Bw.John Mnyika, lilikatika hivyo kusababisha wakazi wa eneo hilo washindwe kupita.

Bw.Sadick alisema, tayari wamewasiliana na uongozi wa mitaa ambayo wananchi wake wameathirika na mvua hizo ili kupata takwimu kamili za watu wanaohitaji misaada.

“Kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kimekutana leo (jana), na tayari tumewaagiza viongozi wa maeneo yaliyoathirika kufanya tathmini ya watu ambao wanahitaji misaada,” alisema.

Aliongeza kuwa, kutakuwa na usimamizi mzuri wa kutoa misaada hiyo kama walivyofanya kwa waathirika wa mabomu Gongolamboto ambapo wale ambao wamekosa sehemu za kulala, watapewa mahema.

Bw.Sadick alisema, leo saa nne asubuhi watatoa takwimu halisi ya watu walioathirika na mvua hizo.





3 comments:

  1. sio kweli hizo helikopta zilizunguka zunguka tu , hakuna mtu aliyeokolewa , msibabaishe wananchi nyie waandishi wa habari feki ili mpate kusifiwa. Haya maafa yanazuilika kama barabara na mifereji ya kupitishia maji itaimalishwa , lakini selikali haina pesa za mambo kama haya ina pesa za kufanyia sherehe za uhulu, muungano , kilismasi , vitamburisho vya uraia , vitamburisho vya uchaguzi.
    harafu ware viongozi wariofika pare wanasema majitu yahame , jee mumewapa sehemu ya kwenda kuishi kwa muda mpaka hayo mamvua yameisha? au munasema sema thuu! Kira mutu anataka lushwa , kwa hio hata hiri janga litakuwa ni uraji kwa wengine ,

    ReplyDelete
  2. serikali inasema watanzania wana vichwa vigumun eti waliambiwa wasijenge lakin wakajenga, je nyinyi kama serikali mliwachukuliaa hatua gani waliojenga!? au mnasubiri maafa muunde tume na kula pesa za misaada??

    ReplyDelete
  3. sasa serikali msifanye mzaha kama wananchi waiishio jangwani walipewa viwanja na vifaa vya ujenzi wakauza halafu wakaendelea kukaa pale pale chakufanya hizo nyumba zote za bondeni zivunjwe pasiwe na mtu wa kurudi

    ReplyDelete