Gabriel Moses na Surah Mushi
SIKU chache baada ya mvua kubwa zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo kuleta maafa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam hasa waishio mabondeni, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imesema mvua hizo zitaendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali nchini na kusababisha maafa hadi mwanzoni mwa Januari 2012.
Akizungumza na Majira jana, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, amesema mvua hizo zitanyesha kwa kasi ya aina yake kutokana na msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo.
Alisema kasi hiyo itasababisha mafuriko na uharibifu mkubwa wa miundombinu hususan barabara, madaraja na makazi ya watu hasa waishio kandokando ya mikondo ya maji na mabondeni.
“Maafa makubwa zaidi yanaweza kutokea kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha kuanzia leo (jana), katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema.
Dkt. Kijazi alisema, mvua hizo zimeanza kunyesha Desemba 28 mwaka huu lakini baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua za kawaida katika kipindi cha mabadiliko ya hali ya hewa.
Miongoni mwa mikoa inayotarajiwa kupata mvua kwa kiwango kikubwa ni Ukanda wa Pwani mikoa Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi na Kisiwa cha Unguja.
Nyanda za Juu Kusini Magharibi mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa, Kanda ya Kati mikoa ya Dodoma, na Singida, Magharibi mwa nchi mikoa ya Kigoma, Tabora na maeneo machache ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Hadi kufikia juzi, watu walioripotiwa kufariki dunia kutokana na mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam, walikuwa 40.
No comments:
Post a Comment