23 December 2011

...amteua Lubuva Mwenyekiti NEC

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amemteua Jaji mstaafu, Damian Lubuva kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Mbali ya uteuzi huo, Rais Kikwete pia amemteua
Jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, kuwa Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo na Bw.Julius Mallaba, kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw.Phillemon Luhanjo, imesema uteuzi huo umeanza  Desemba 19, mwaka huu.

Kabla ya uteuzi huo, Bw.Lubuva alikuwa Jaji katika Mahakama ya Rufani Tanzania na baada ya kustaafu, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili ya Viongozi.

Bw.Lubuva anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Lewis Makame ambaye mkataba wake wa utumishi wa umma umekwisha Julai, mwaka huu.

Kwa upande wake, Jaji Hamid alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kabla ya kustaafu kwake akichukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Jaji Omari Makungu.

Jaji Makungu aliteuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadaye akateuliwa kuwa Jaji Mkuu.

Bw.Mallaba, kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkurugenzi wa Sehemu ya Mikataba katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.  

Nafasi aliyochukua ilikuwa ikishikiliwa na Bw.Rajabu Kiravu ambaye amemaliza mkataba wake wa utumishi Septemba, mwaka huu.



1 comment: