25 November 2011

ZUIO LA MAANDAMANO:

Jukwaa la Katiba lajibu mapigo

*Lasema maandamano ni Haki ya Watanzania

Na Rachel Balama

JUKWAA la Katiba Tanzania ambalo linajumuisha asasi za kiraia zaidi ya 180 vikiwemo vyama vya wafanyakazi, wanataaluma, waishio na VVU/UKIMWI, vyama vya
wanafunzi na Taasisi za Kiimani Tanzania Bara na Zanzibar, limesema pamoja na kusitishwa kwa maandamano ambayo awali yalipangwa kufanyika kesho, watapanga tarehe nyingine ili kutekeleza azma hiyo.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Bw. Deus Kibamba, imesema kusitishwa kwa maandamano hayo kulitokana na ombi la Jeshi la Polisi nchini lakini lengo la kumsihi Rais Jakaya Kikwete kutotia saini Muswada wa Mabadiliko ya Katiba 2011, lipo pale pale.

Alisema maandamano ni haki ya raia wa Tanzania kwa mujibu wa katiba kama njia moja wapo ya kutoa maoni yao ambapo wajibu wa Jeshi la Polisi ni kusimamia amani na usalama wa wananchi ili kuhakikisha wanapata haki hiyo.

“Visingizio vinavyotumika ili kuwanyima haki Watanzania havikubaliki kwa sasa hata siku za usoni, Jeshi la Polisi lina wajibu wa kupanga ratiba ambayo itawezesha wananchi kupata haki ya kuandamana bila kuingiliwa au kuvurugwa na mtu,” alisema.

Aliongeza kuwa, hali inayocheleweshwa ni sawa na haki inayonyimwa hivyo wajibu wa jeshi hilo ni kutoa haki ya kikatiba kwa wakati badala ya kuichelewesha. Alisema jukwaa hilo litaendelea kuwa mstari wa mbele kudumisha amani kwa njia mbalimbali ikiwemo kuandaa mikutano, mijadala, midahalo, semina na maandamano kwa ajili ya wananchi kupata fursa ya kutoa maoni na madukuduku yao kuhusu mchakato na maudhui ya katiba mpya.

Aliongeza kuwa, viongozi wa jukwaa hilo walikubaliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema, kujadiliana namna ambavyo maandamano hayo yangetekelezwa.

Alisema katika kikao hicho, IGP Mwema aliomba jukwaa hilo lisitishe maandamano yaliyopangwa kufanyika kesho kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kupokea maombi ya kaundi mengine ya kijamii na kisiasa kutaka kufanya maandamano nchi nzima siku hiyo hiyo hivyo kuleta mkanganyiko wa ratiba.

“Polisi walisema kama tungefanya maandamano, upo uwezekano mkubwa wa kutokea mtafaruku kwa waandamanaji wa pande mbili zinazopishana kimtazamo juu ya muswada huu, kundi moja likiunga mkono na jingine likipinga muswada huu.

“Jukwaa litapanga tarehe nyingine ya maandamano kwa mawasiliano na Jeshi la Polisi na kuyatangaza kwa wananchi wote katika siku za usoni kama Rais Kikwete atatekeleza nia yake ya kuusaini muswada huu,” alisema.
Aliongeza kuwa, muswada huo haukupata nafasi ya kujadiliwa na wananchi ambao ndio wamiliki wakuu wa katiba na mchakato wote wa kujenga na kuandika katiba mpya.

5 comments:

  1. Nyie wanaharakati mbona hatuwaoni mahakamani kutetea na kufuatilia dhuluma wanazofanyiwa walalahoi huko. au kazi yenu ni siasa tu kwa niaba ya chadema?

    ReplyDelete
  2. "****Nyie wanaharakati mbona hatuwaoni mahakamani kutetea na kufuatilia dhuluma wanazofanyiwa walalahoi huko. au kazi yenu ni siasa tu kwa niaba ya chadema?***"

    Nadhani usuburi si siku nyingi tutaona wannchi wakiingia mahakamani na kufanya vitu vyao. Dhuluma wanazofanyiwa wananchi zina ukomo wake. Wote tunajua kuwa Polisi na mahakama wamekubuhu katika rushwa. Iko siku watu watachukua sheria mkononi hata huko mahakamani. Wote tumeshuhudia wannchi wnavyoanza kupambana na Polisi.

    Serikali inabidi isome vizuri ishara za nyakati na kuchukua maamuzi makubwa.

    ReplyDelete
  3. Maandamano ni haki ya raia kwa mujibu ya katiba ya sasa, Hivyo serikali isiwatishe watu kudai haki zao! Wasiwas na uzoefu unaonesha kuwa hawa viongozi hasa wanaojidai ni wanaharakati hawajitokezi ktk maandamano yenye ishara ya kupigwa mabomu,wao hujitokeza ktk maandamano ya amani, na kufanya walalahoi kuumia zaidi, wanatakiwa kuiga toka Misri, sio hawa wabongo wamekaa kimsalahi ya kiN.G.O tu.

    ReplyDelete
  4. Inaonekana NGO nyingi sasa zimeshindwa kufanya kazi zao za msingi, wameamua kuingia katika ulingo wa harakati za kisiasa. KARIBUNI SANA.

    ReplyDelete
  5. NDIO MAANA ZITTO KABWE AKASEMA NCHI HAINA MAWAZIRI WANAODFANYA KAZI. HIVI HIZI NGO SI ZINA KATIBA ZAO AMBAZO ZINAWEKA BAYANA MIPAKA YA SHUGHULI ZAO NA WAJIBU WA KUTOJIHUSISHA NA SIASA. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YUPO WAPI AANZE KUWAHOJI HILI LA KUANDAMANA KUPINGA KUUNDWA KWA KATIBU KWA MUJIBU WA SHERIA NA KATIBA WANAYOIDAIA HAKI, YUPO WAPI? TUSHAKUWA SHAMBA LA BIBI, AU KICHWA CHA MWENDAWAZIMU KIASI HIKI?

    ReplyDelete