21 November 2011

Watimuliwa kufanya mitihani kwa kukosa ada

Na Salim Nyomolelo

ZAIDI ya wanafunzi 100 wa kidato cha kwanza na cha tatu katika Shule ya Sekondari Kwamkono wilayani Handeni mkoani Tanga wamezuiliwa kufanya mitihani yao ya mwisho wa mwaka kwa kushindwa kukamilisha michango mbalimbali ikiwemo ada.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu wiki iliyopita, mmoja wa wazazi wa mwanafunzi anayesoma katika shule hiyo alisema uongozi wa shule hiyo ilifikia uamuzi huo bila kuwashirikisha wazazi wao ambao ndio watafutaji wa fedha.

Alisema Mkuu wa shule hiyo Bw. Francis Msaba, aliwafuata watoto wao walipokuwa madarasani wakijiandaa kufanya mtihani wa uraia na kuwatoa kurudi nyumbani kutafuta fedha bila kuzingatia kuwasiliana na wazazi au walezi amboa ndio watafutaji wa fedha.

"Rais Jakaya Kikwete, alipoingia madarakani alituhakikishia wananchi kuwa hakuna watoto wa masikini ambao watarudishwa nyumbani kwa kukosa ada, leo hii tunaona wazi watoto wetu wanarudishwa nyumbani na kukosa kufanya mitihani ikiwa wao sio watafutaji wa pesa;

"Mwanafunzi anaporudishwa nyumbani kusubiria ada anarudi nyuma kitaaluma, mwalimu anakuwa anaendelea kufundisha waliobaki bila kujali wasiokuwepo, hii inawafanya watoto wa wakulima kama sisi kutopata elimu,lakini kinachonishangaza ni kauli ya rais kutotekelezwa na watendaji wa chini," alisema mzazi huyo huku akisisitiza jina lake kuhifadhiwa.

Alisema wao kama wazazi wanasikitishwa na kitendo cha watendaji wanaomsaidia rais kama mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kujisahau mara kwa mara kuwajibika kutekeleza ahadi za kiongozi huyo wa nchi badala yake wamekuwa wakiwachanga wananchi.

Alisema kitendo hicho kinaweza kusababisha wanafunzi hao kufanya vibaya katika masomo yao hivyo kurudisha nyuma juhudi za serikali kuhakikisha kila mwanafunzi anapata haki yake bila kujali uwezo wa mzazi au mlezi wake.

Naye mzazi mwingine Bi. Mwajabu Mohamed, mwenye watoto wawili katika shule hiyo alisema amesikitishwa na watoto wake wawili aliowataja kuwa ni Nasri Juma na Husna Juma kuzuiwa kufanya mtihani kwa kudaiwa sh.100,000.

"Sikutaka kuzungumzia suala hili.... lakini niseme tu ukweli nimesikitika sana, sikukataa kulipa hizo fedha lakini nilikuwa nawalipia na wengine waliokuwa wakihitimu hivyo ni lazima wao kwanza niwakamilishie wasibaki na deni kisha nakamilisha kwa hawa baadaye kwa kuwa bado wapo shuleni ila imeniuma sana wamefukuzwa kufanya mtihani,"alilalamika Bi. Mohamed.

Majira ilipomtafuta mkuu wa shule hiyo kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia suala hilo alisema hayupo tayari kutoa taarifa yoyote na kumtaka mwandishi wa habari hizi kufika katika shule hiyo.

Alipoulizwa kukanusha au kukubali kuwepo kwa wanafunzi waliozuiliwa kufanya mitihihani hiyo shuleni kwake alisema "Nimesema siko tayari kusema lolote wewe njoo huku ukitaka,"alisema Bw. Msaba na kukata simu.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Handeni Bw.Simon Mdaki, alisema hadi mwishoni mwa wiki alikuwa hajapata taarifa hizo kiofisi huku akiungana na mkuu wa shule kumtaka mwandishi wa habari hizi kufika katika shule hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi walikiri kufukuzwa na kushindwa kufanya mitihani yao kwa kushindwa kulipa ada na michango mbalimbali ya shule.

"Kwa mfano mimi sikufanya mtihani wa civics (Uraia) ulioanza kwa siku ya kwanza, baada ya kulipa nimefanikiwa kuanza kufanya masomo yanayofuata ila wenzangu wengi tu bado wamezuiliwa," alisema mmoja wa wanafunzi wa shuleni hapo jina tunalo.

Akizungumzia hali hiyo Mkuu wa Kitengo Cha Habari, Elimu na Mawasiliano Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bi. Magdalena Kishiwa, alipoombwa na gazeti hili kutoa ufafanuzi wa kifungu cha sheria kinachomruhusu mkuu wa shule kuwafukuza wanafunzi kipindi cha mtihani kwenda kutafuta ada alisema kufanya hivyo ni kinyume cha utaratibu.

Alisema kuwafukuza wanafunzi kipindi cha mitihani kwa sababu ya kukosa ada ni kosa kisheria na kuweka wazi kuwa hakuna sheria inayomruhusu mkuu wa shule kufanya hivyo na kuahidi kufuatilia suala hilo.

Hata hivyo aliwataka walimu, wazazi na walezi kutimiza wajibu wao mapema kabla ya kipindi cha mitihani na kuwa na mahusiano mazuri kutatua changamoto mbalimbali kwa lengo la kuwapatia wanafunzi elimu bora na kukwepa kuwaathiri kisaikolojia hususan kipindi cha mitihani.

No comments:

Post a Comment