28 November 2011

Wataka barabara ya lami kwenda hospitali

Na Eliasa Ally, Iringa

WANANCHI wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wameitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuitengeneza kwa kiwango
cha lami barabara yenye urefu wa kilomita 4.5 inayokwenda katika Hospitali Teule ya wilaya hiyo ya Tosamaganga ili kuwawezesha kuufikia kwa urahisi.

Wamesema eneo la barabara hiyo inayoanzia njiapanda ya Kalenga ni mbovu hivyo kuwasababishia athari kubwa wakati hospitali hiyo ndio msaada mkubwa kwa wakazi wa mjini na maeneo ya vijijini ambao wanapatiwa huduma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wananchi walisema licha ya Hospitali Teule ya Tosamaganga kufanya kazi vizuri na kuwafanya watu wengi wanahitaji huduma za matibabu kuukimbilia,tatizo kubwa ni kipande hicho cha barabara cha kilomita 4.5 cha changalawe.

Walisema Manispaa ya Iringa imefanikisha kuwa na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 16 kutoka mjini hadi kijiji cha Kalenga lakini kipande hicho cha kilomita 4.5 kinawaletea usumbufu kutokana na baadhi ya wagonjwa mahututi kusafirishwa kwa shida.

Walisema kutokana na ubovu wa kipande hicho cha barabara nauli imepanda kutoka sh. 500 waliyokuwa wakilipa awali hadi kufikia sh. 2,000 hali  inayowangezea gharama za maisha.

"Eneo hili la Iringa hatuna hospitali nyingine ambayo ni tegemeo kubwa kama
hospitali ya Tosamaganga, kinachotuumiza zaidi ni ubovu wa barabara, ni kipande kidogo tu cha kutengenezwa kwa kiwango cha lami chenye kilomita nne na nusu ikitengenezwa nauli zitapungua," alisema Bw. Fabiani Nyaulingo, mkazi wa Tosamaganga.

Akizungumzia hali ya kipande cha barabara hiyo Mbunge wa Kalenga Dkt. William Mgimwa, aliungana na wananchi hao na kuongeza kuwa barabara hiyo ni muhimu kutengenezwa kutokana na hospitali ya Tosamaganga
kuwa tegemeo katika huduma za afya.

No comments:

Post a Comment