28 November 2011

NCCR wamwonya JK mchakato wa Katiba

Na Peter Mwenda

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimetoa tamko rasmi kuhusu muswada wa sheria ya kuundwa kwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi
kuhusu katiba Mpya na kumshauri Rais Jakaya Kikwete, kutosaini muswada huo kuepusha taifa kuingia kwenye malumbano.

hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Taifa Bw. James Mbatia, wakati akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho Jijini Dar es Salaam.

Alikumbushia historia ya kupigania mabadiliko nchini na kusema kuwa NCCR Mageuzi ilikuwa ya kwanza kuwasilisha mapendekezo ya Katiba Mpya ya Tanzania kwa Rais Kikwete mwezi Aprili mwaka huu lakini cha kushangaza mpaka sasa hajaitwa wala kujibiwa.

Bw. Mbatia aliweka wazi kuwa chama chake inaona giza likikumba Taifa kutokana na ukweli kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haipo kisheria wala kihalisia kutoka na kitendo cha Tanzania Zanzibar kubadili katiba yao na kusema kuwa eneo hilo ni nchi.

"Wanzanzibari hawatataliwa na kura ya maoni ya sheria ya muungano kwa kuwa wanayo sheria yao ya kura ya maoni, katiba ya Zanzibar haibadilishwi bila kura ya maoni iliyopigwa kwa mujibu wa sheria na Zanzibar kuridhia," alisema Bw, Mbatia.

Alisema kabla ya Rais Kikwete kukubali hoja ya kuwa na mchakato wa kuandika upya katiba kumekuwa na viashiria vinavyoonesha kuwa kumekuwepo na utayari na dhamira ya kweli ya CCM na serikali yake kukataa dhana nzima ya katiba mpya.

Alisema CCM hakioni umuhimu wa kuandika katiba mpya ndiyo maana hawataki kubainisha kwenye ilani yao ya uchaguzi na kwamba hata baada ya rais kukubali bado inaonekana CCM na serikali yake kuhakikisha mchakato mzima unakuwa mikononi mwa dola.

Mwenyekiti huyo alisema mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi unaanzishwa nchini NCCR Mageuzi ni miongoni mwa vyama vilivyoanzishwa kuhoji uhalali wa Katiba ya Tanzania kwa nguvu nyingi na kubainisha madhaifu makubwa.

Alisema NCCR Mageuzi ndiyo waasisi wa kudai Katiba ya Tanzania na kwamba wanayo imani kubwa kuwa watanzania wanao uwezo wa kujipatia katiba wanayoitaka kwa kuandikwa katiba mpya.

Bw. Mbatia alitaja baadhi ya kasoro katika muswada huo kuwa ni pamoja na vifungu vya 28 na 29 cha sheria mpya kuonesha kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo chombo kinachosimamia kura ya maoni huku wengi wakikosa imani na tume hiyo kwa sasa kutokana na kutokuwa huru.

Alisema kifungu cha 26 kinaonesha kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya kuhakikisha Bunge la katiba linakuwa chini yake na kuongeza kuwa NCCR-Mageuzi inapendekleza Bunge la Katiba kuwa huru ili kufanya kazi yake bila shinikizo na mtu au kikundi chochote.

Alisema kifungu cha 20 cha sheria mpya kinabainisha kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya kuteua wajumbe 116 kutoka Asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na kwamba chama chake kinapendekeza kuwa wawakilishi hao wateuliwe na taasisi husika badala ya ya Rais.

Bw. Mbatia alisema NCCR Mageuzi inafahamu kuwa msingi wa umasikini unaokabili watanzania ni mfumo mbovu wa utawala hivyo katiba ya nchi ndiyo silaha ya kuhakikisha kunafanyika mapinduzi ya kisasa.

1 comment:

  1. Ifikie wakati hili suala la serikali tatu likubaliwe. Nasema hivyo kwa sababu Zanzibar wana mamlaka yao na yale yanayowahusu wanaamua wenyewe bila kushirikisha bara. Lakini cha ajabu ni kwamba yanayohusu Bara Wazanzibar wanashirikishwa hapo bado naona giza ni kwa nini? Iwepo Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar halafu Jamhuri ya Muungano ili Watanganyika nao waamue ya kwao peke yao kama Wazanzibar wanavyoamua ya kwao peke yao. Huu muungano upo kama vile ni maslahi ya watu fulani.

    ReplyDelete