Na Salim Nyomolelo
BAADHI ya wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu wilayani Temeke (CHAWATE SACCOS), wameilalamikia ofisi ya ushirika wilayani
humo kwa madai ya kushindwa kusimamia sheria za uendeshaji wa chama hicho.
Wanachama hao wamesema hali hiyo imechangia chama hicho kukumbwa na mgogoro ambao umedumu muda mrefu hadi sasa.
Wakizungumza na Majira hivi karibuni kwa masharti ya kutotaja majina yao gazetini, baadhi ya wanachama hao wamesema kuwa, matatizo mengi yanayohusu chama hicho yamekuwa yakifikishwa katika ofisi hiyo lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
“Kimsingi tumechoshwa na viongozi wetu ambao wanakiuka sheria na taratibu za uendeshaji wa SACCOS, Mwenyekiti wa chama hiki ni Bw. Ebrahim Mketo ambaye ni mwalimu mstaafu.
“Kwa mujibu wa katiba ya chama, Bw. Mketo hapaswi kuendelea na wadhifa alionao kama Mwenyekiti wa Bodi kwa sababu hana namba ya TSD kama taratibu zinavyosema,” walisema walimu hao.
Waliongeza kuwa, Bodi hiyo ilichaguliwa Mei 2010 ambapo Bw. Mketo, alistaafu kazi Juni 30,2010 hivyo wanachma waliamini kuwa, Desemba 2010 Mwenyekiti huyo angetangaza kujiuzulu wadhifa alionao katika uchaguzi mkuu lakini hakufanya hivyo.
“Huyu Mwenyekiti alikopa sh. milioni 10 badaya ya sh. milioni 3.2 kulingana na akiba yake ya sh. milioni 1.6 kwani katiba inamtaka mwanachama akope mara mbili ya akiba yake.
“viongozi wengine wa SACCOS wananyanyasa wanachama kwa madai wapo karibu na viongozi wa ushirika hivyo hawawezi kuchukuliwa hatua, jambo hili limesababisha wanachama kupoteza imani na viongozi wa ushirika,” walisema.
Waliongerza kuwa, viongozi hao walichukua mkopo kutoka Pride bila kuwashirikisha wanachama kama katiba inavyosema pamoja na walimu kuzungushwa wanapotaka mikopo.
Kutokana na hali hiyo, wanachama hao wameitaka bodi hiyo kujiuzulu ili chama hicho kipate viongozi wapya kwani pamoja na wanachama kukataa bajeti iliyopendekezwa, viongozi hao wamepuuza msimamo wao na kuendelea kuitumia.
“Tunauomba uongozi wa juu ya Wilaya uingilie kati suala hili, tunahitaji mkutano mkuu wa dhalula ambao utahudhuriwa na Mkurugenzi wa Manispaa ili tuweze kutoa kero zetu,” walisema.
Akijibu tuhuma hizo, Bw. Mketo alikanusha madai hayo na kusema kuwa, wakati akichaguliwa katika nafasi hiyo, hakukuwa na sheria inayomtaka mwalimu mstaafu kutogombea uongozi katika chama.
“Hii SACCOS ina wanachama wastaafu zaidi ya 20 ambao kwa mujibu wa taratibu, wataendelea kuwa wanachama na wana haki ya kuchagua viongozi na kuchaguliwa.
“Sheria ya 1995 inaeleza wazi kuwa, mwanachama wa SACCOS anaweza kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi katika chama kama an hisa katika chama,” alisema Bw. Mketo.
Akizungumzia mkopo aliochukua, Bw. Mketo alisema hajawahi kuchukua mkopo tangu aingie madarakani na kumtaka Mwandishi amuulize Mwenyekiti wa Mikopo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mikopo katika SACCOS hiyo, Bw. Kassimu Wambonaheri, alisema tangu ashike nafasi hiyo mwaka 2008 hadi sasa, hajawahi kupitisha jina la Bw. Mketo kwa maombi ya mkopo.
Faili la mikopo katika ofisi hiyo, linaonesha kuwa Bw. Mketo alikopa sh. milioni sita Mei 21,2008 na sh. 400,000 Aprili 2011, tofauti na majibu yaliyotolewa na Bw. Mketo pamoja na Bw. Wambonaheri. Majira lilipotaka kujua Bw. Mketo anamiliki hisa kiasi gani ilidaiwa anamiliki sh. milioni 3.1.
Akijibu hoja ya SACCOS hiyo kukopa Pride bila kushirikisha wanachama, Bw. Mketo alikiri chama hicho kukopa sh. milioni 200 na kuongeza kuwa, walitumia ubunifu kwa sababu chama hicho hakikuwa na fedha wakati wanachma wanataka mkopo.
Ofisa Ushirika wilayani humo, Bi. Jenipher Katua, alisema malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya walimu hayajamfikia na kuongeza kuwa, wanacham hao ni kundi ndogo lenye maslahi binafsi.
Akizungumzia ukaribu wake na viongozi wa SACCOS hiyo Bi. Katua alisema madai hayo hayana ukweli wowote kwani Mwenyekiti huyo walimchagua wenyewe wakijua anakaribia kustaafu.
“Katika huo uchaguzi, Bw. Mketo alimpita mpinzani wake kwa zaidi ya kura 400 sasa utaona ni jinsi gani walivyokuwa wanamkubali,” alisema Bi. Katua.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Bi. Margareth Nyalile, alisema malalamiko ya walimu hao hayajamfikia ila yupo tayari kushiriki mkutano mkuu ambao utaandaliwa ili kusikiliza kero zao.
No comments:
Post a Comment