25 November 2011

Vyama vya Siasa vyatofautiana kukutana na Rais Kikwete

Na Rabia Bakari

USHAURI wa Kamati Kuu (CC), ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka Rais Jakaya Kikwete akutane na vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni ili
kusikiliza mawazo yao juu ya mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya, umepokelewa kwa hisia tofauti na wawakilishi wa vyama husika.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Katibu Mwenezi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mwenyekiti wa Wabunge wa chama hicho na Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila, alisema uamuzi huo wa CC hauna mantiki yoyote. ‚Binafsi sioni sababu ya kukutana na Rais Kikwete wala sitegemei lolote kutoka katika kikao hicho, sisi hatukutoka bungeni ili tukutane na rais baadaye.

“Sisi tunaamini CCM, Serikali pamoja na rais hawana dhamira ya kweli katika muafaka wa agenda ya Katiba tangu mwanzo kwa sababu katiba wanayotaka wananchi ni msumali kwa chama tawala na serikali yake,” alisema.

Aliongeza kuwa, ushahidi kuwa Serikali haiko tayari kwa jambo hili upo wazi kwani CCM tangu awali ilikataa kuweka agenda ya katiba mpya katika ilani yao mwaka 2010 ingawa msukumo wa umma ulikuwa mkubwa.
Pili Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Waziri wa Sheria na Katiba, Bi.Celina Kombani, walishasema awali kabla ya tamko la Rais Kikwete kuwa, jambo hilo halina umuhimu wowote kwa sasa na hawajafuta kauli yao.

Tatu Aprili mwaka huu, Rais Kikwete alipitisha muswada mbovu kuliko yote kiasi cha kuamsha hasira ya umma kuchana muswada huo na kutakiwa urejeshwe serikalini.

Nne hata uliporejeshwa na ukaletwa mpya, bado serikali na CCM wakashinikiza bunge lijadili na kupitisha kabla ya umma kupata nafasi ya kujadili kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa kanuni.
Tano uamuzi baada ya Rais Kikwete kusikia kilio cha jamii na wanaharakati nje ya siasa, aliamua kukutana na wazee wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam na kusisitiza msimamo wake na chama chake kuthibitisha kuwa hawako tayari kwa mchakato wa katiba wanayotaka Watanzania.

“Huu ni ushahidi tosha kuwa katiba wanayotaka Watanzania haiwezi kutoka mikononi mwa CCM kwa majadiliano na hoja hivyo sisi tunajipanga kwa namna mbadala kuhakikisha mwisho wa siku Watanzania wanapitisha katiba wanayotaka na sio vinginevyo.
Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Bw.Augustino Mrema, amepongeza ushauri wa CC kutaka Rais Kikwete akutane na vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni.

“Awali sisi tulikutana na Rais, CHADEMA wakasema tumehongwa, tumenunuliwa sasa sijui wao huo ujasiri wa kukutana na Rais Kikwete wameupata wapi,” alihoji Bw. Mrema.
Alionya kuwa unafiki kwa jamii ni kitu hatari sana na kuwataka CHADEMA kuwa na msimamo unaoeleweka.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mkurugenzi wa Siasa wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Mbaralah Maharagande, alisema uamuzi huo wa CCM umechelewa kwani walitakiwa kuufanya mapema.
“Mazungumzo ndiyo msingi wa amani na kufikia mafanikio, kama CCM na CHADEMA wangekubali kufanya mazungumzo mapema kwa kuhusisha pia vyama vingine kama ilivyopendekezwa, hali ya misukosuko ya kisiasa na msuguano wa katiba mpya uliopo sasa usingefikia hatua hii lakini wamesubiri mpaka muswada umepitishwa bungeni ndipo mkutano na Rais ufanyike, wamechelewa kwa kweli,” alisema.
Mwenyekiti wa chama cha UPDP, Bw.Fahmi Dovutwa, alisema haoni umuhimu kwa kuwa CCM na Serikali yake walilala muda mrefu.

Alisema hatua iliyofikiwa na CCM ni mbaya kwa kuwa hawana moyo wa uzalendo na udugu kwa vyama vya siasa hivyo kinachofanyika katika mkutano huo ni hadaa

No comments:

Post a Comment