25 November 2011

NEC-CCM yamkaanga Ng'enda

Na pendo Mtibuche, Dodoma

HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC), Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeanza kuonesha makali yake baada ya Bw. Kilimbe Ng’enda kuvuliwa ukatibu wa chama hicho
Mkoa wa Dar es Salaam kwa kosa la kwenda kinyume na maamuzi ya vikao vya chama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, alisema Bw. Ng’enda, alikwenda kinyume na vikao halali vya chama kuhusu suala la uchaguzi wa madiwani wa viti maalumu.

“Kimsingi Bw. Ng’enda atapangiwa kazi nyingine, kikao tulichoanza jana, kinaendelea vizuri, lengo letu leo (jana), tumalize shughuli zote zilizopangwa,” alisema.

Akizungumzia taarifa iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuhusu ratiba ya uchaguzi mdogo katika Jimbo la Uzini, Bw. Nnauye alisema kwa kuzingatia ratiba hiyo, wamekubaliana kuwa, Novemba 28 hadi Desemba 2 mwaka huu, itakuwa siku ya wana CCM kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo.

“Kamati kuu itakutana Januari saba hadi nane kuteua jina la mgombea wa kiti hiki, kesho (leo), Mwenyekiti wa CCM , Rais Jakaya Kikwete, atafungua semina ya siku tatu ya watendaji wa chama ngazi ya wilaya hadi taifa,” alisema Bw. Nnauye.

Alisema lengo la semina hiyo ni kujadili njia za kufanikisha shughuli za utendaji ndani ya chama. Taarifa zilizotufikia wakati tukienda mtamboni zinasema kuwa, kikao hicho kilimalizika saa moja kasoro usiku ambapo Bw. Nnauye alisema kuwa, taarifa juu ya kilichojiri katika kikao hicho, zitatolewa leo saa tano asubuhi.

3 comments:

  1. cc na viongozi wa juu wa ccm watajipongeza lakini huyu n'genda ni dagaa tu mapapa na manyangumi bado wanapeta. changa la macho tu!

    ReplyDelete
  2. CCM hawawezi kuvua Gamba kwa kuwa wote ni wachafu.Wanaogopa kuvuana nguo hadharani,kuvua gamba kwao maana yake ni CHAMA KUFA kwakuwa hakuna hata mmoja aliye msafi.Cha ajabu ni kwamba hawa wanataka eti kututengenezea katiba mpya kupitia mwenyekiti wao.Ukweli ni kwamba KATIBA haiwezi kuwa safi pia.

    ReplyDelete
  3. Acheni umbumbumbu, katiba haitengenezwi na rais wala taasisi moja au mtu mmoja. Wananchi ndio wanatakaotoa maoni yao katiba yao iweje na sio rais pekee. Kwa upotoshaji huu ndio maana hatutafika haraka huko tuendako.Unategemea mtu asemaye uongo siku zote kwa maslahi yake binafsi awe mtawala, si ataendelea na uongo wake ili mradi atimize malengo yake binafsi. Kusema uongo ni dalili za kiongozi mbaya.

    ReplyDelete