Katibu Mkuu Ardhi apokea vitisho
Neema Malley na Jane Hamalosi
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Patrick Rutabanzibwa, amesema amekuwa
akipokea simu za vitisho kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa wakimiliki maeneo ya wazi ya viwanja.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Rutabanzibwa alisema alikuwa akipigiwa simu kila mara na watu asiowafahamu na kutishiwa kuwa atauawa yeye pamoja na watendaji wenzake.
Bw. Rutabanzibwa alisema kuwa hakuwa na hofu ya tishio hilo, bali aliwajibu kuwa kifo ni mipango ya Mungu na yeye pamoja na wenzake hawataacha kutetea suala hilo, ili kulinda haki na usawa kwa wote.
"Sitishiki kwa vitisho vya kuuawa kwa kuwa kifo ni kitu cha kawaida kwa binadamu yoyote na pia ni mipango ya Munguuadilifu kwa faida ya jamii nzima," alisema Bw. Rutabanzibwa.
Alisema vitisho vilitokana na watu wanaochukua maeneo ya wazi bila kujua sheria au kutokana na utovu wa nidhamu na serikali inapomwambia kuwa amekosea basi anaanza kutoa vitisho kwa wahusika wanaosimamia sekta hiyo.
Alisema kuwa hatotishika kutokana na vitisho hivyo, kwa kuwa havikuanza leo wala jana kwani alipokuwa katika Wizara ya Miundombinu aliwahi kupigiwa simu kama hizo, lakini hadi leo hakuna kinachoendelea na simu hizo hazijabadilisha msimamo wake.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, alisema tayari wizara yake imeingia katika kesi na Kampuni ya Kahama Mining.
Alisema kuwa kampuni hiyo ilichukua eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kujenga ya kujenga shule.
Alisema kuwa wizara hiyo iligoma kutoa hati ya umiliki kwa Kampuni ya Madini ya Kahama kwa viwanja vya Oysterbay na viwanja hivyo vimepona kwa kuokolewa na wizara yake.
Eneo hilo la wazi liligawiwa na Manispaa ya Kinondoni Oktoba 20, 2009, kitendo ambacho kilielezwa uamuzi huo wa manispaa ni uzembe na ukaidi kwa waziri.
Alisema kuwa eneo hilo tayari limejengwa Shule ya Sekondari ya Bogoyo na kampuni hiyo itatafutiwa sehemu nyingine.
Pia Prof. Tibaijuka aliishauri jamii kujua sheria za ardhi kwa kuwa wasipozijua wataishia kudhulumiwa.
Hata hivyo alisema kuwa wizara yake ina mpango wa kuweka ramani za mipango miji katika maeneo yote.
Aidha Prof. Tibaijuka alisema hata viwanja vya Jangwani havitambuliki na watu wa eneo hilo wanaishi kwa matumaini na wakati wowote wataondolewa.
Prof. Tibaijuka katika ziara yake ya kwanza ya kutembelea maeneo ya wazi yaliyoporwa na kuendelezwa kinyume cha utaratibu alikwenda Sinza, Vatican jijini Dar es Salaam ambako alikuta kiwanja cha wazi kimeuzwa kwa sh. mil. 500.
Mhusika aliyeuziwa eneo hilo ambalo lilitengwa kwa ajili ya burudani na michezo, Bw. Primi Aloyce Mushi, alisema alinunua eneo hilo Septemba mwaka huu kutoka kwa watoto wa familia moja kwa sh. mil. 500.
Inadaiwa kuwa baada ya kusikia tangazo la Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa eneo hilo lisiendelezwe kwa kuwa ni mali ya serikali, lililotengwa kwa ajili ya michezo, vijana hao walitafuta mteja haraka na kuliuza.
"Waziri nimekuelewa sana unayosema ni ufafanuzi wa kutosha, lakini ni kweli kuwa tumeuziwa eneo hili hivi karibuni ni juzi tu, hata miezi mitatu haijaisha kwa sh. mil. 500, waliotuuzia ni vijana wa huyu mzee wa hapa ambaye ni marehemu," alisema Bw. Mushi.
Profesa Tibaijuka akifafanua kuhusu maeneo ya wazi alisema Mkurugenzi wa Mipango Miji, Bi. Albina Bura alipaswa kujua kila eneo la wazi na linahusika kwa ajili ya matumizi gani na si kama inavyofanywa na wajanja wachache kuchakachua ramani za kukopi na kuhadaa wananchi kuuza maeneo kama hayo.
"Huu ni udanganyifu, mbele ana kiwanja halali kidogo lakini eneo jingine ni la wazi la serikali hivyo anatumia ramani halali kuuza kiwanja cha wazi,serikali za mitaa, madiwani, wabunge na mawaziri kazi yetu ni kuelimisha jamii kuhusu ardhi," alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema wizara yake itajiandaa kuchapisha ramani halisi na kuzigawa nchi nzima kwa ajili ya kuziuza ili kila mwananchi ajue eneo analotaka kununua kama la wazi na limetengwa kwa ajili ya matumizi gani.
Profesa Tibaijuka alisema wizara yake haitarudi nyuma kutwaa maeneo yote ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali na baadaye kuvamiwa na watu na kubadilisha matumizi yaliyokusudiwa.
Alisema maeneo yaliyovamiwa na kuwekwa gereji na matumizi mengine ni muhimu kwa jamii lakini serikali itawatengea maeneo husika kwa ajili ya kazi husika.
Alisema maofisa katika wizara yake watapita mara kwa mara katika maeneo ya wazi ambayo wameweka mabango ya kuzuia kuendeleza viwanja vya wazi ili kusisitiza wahusika waondoke na kuwahadharisha majirani wa maeneo hayo wasije kuuziwa na kupata hasara.
HONGERA TIBAIJUKA, LAKINI MBONA DAR TU. NENDA NA MIKOANI UKATOE UOZO ULIOPO.
ReplyDeleteHongera mama mchapakazi lakini serikali ilibidi itoe tadhali mapema kabla wanachi awajayaendeleza maeneo husika kuliko kusubiri mpaka wananchi wanaingia hasara zaidi.
ReplyDelete