08 November 2011

Twanga yazindua albamu ya 11

Na Victor Mkumbo

BENDI ya muziki wa dansi nchini, The African Stars'Twanga Pepeta' juzi ilizindua albamu yake ya 11 katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Bendi hiyo ilizindua albamu yake ya Dunia Daraja ambayo yenye nyimbo sita, ambazo zimetungwa na wasanii wa Twanga.

Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Dunia Daraja uliobeba jina la albamu, Penzi la Shemeji, Umenivika Umasikini, Mtoto wa Mwisho, Kauli na Kiapo Cha Mapenzi.

Katika uzinduzi huo, bendi za Msondo Ngoma, Mashujaa Musica, Mashauzi Classic na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Mataluma, walisindikiza na kuzikonga nyoyo za mashabiki waliohudhuria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Kampuni African Stars Entertainment Tanzania (ASET), Asha Baraka alisema kuwa,  uzinduzi huo ni sehemu ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Alisema baada ya uzinduzi huo wanatarajia kufanya maonesho katika mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi.

“Tunatarajia kufanya maonesho mbalimbali ya bendi yetu ili mashabiki wetu wapate burudani na kuzisikia nyimbo zetu mpya,” alisema.

No comments:

Post a Comment