17 November 2011

Tenga akiri Stars kucheza 'fyongo'

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amekiri timu ya taifa (Taifa Stars), kucheza chini ya kiwango katika mchezo dhidi ya Chad, licha ya kufuzu kucheza hatua ya awali ya makundi ya kuwania kucheza Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Mbali na hilo, Tenga amemsifia beki Shomari Kapombe kwa jinsi alivyocheza na kumtabiria kuifanyia makubwa timu hiyo.

Akizungumza wakati wa upangaji wa ratiba ya michuano ya Kombe la Chalenji Dar es Salaam jana, Tenga alisema anaishukuru timu hiyo kwa kufuzu hatua ya makundi na ana imani itafanya vizuri katika hatua hiyo.

"Unajua mchezo wa soka ndivyo ulivyo, tumeshinda ugenini 2-1 lakini cha kushangaza tumefungwa nyumbani 1-0, lengo letu ya kushiriki mashindano haya ni kusonga mbele na hilo limefanyika," alisema Tenga na kuongeza;

"Pamoja na kwamba tumevuka lakini timu haikucheza kama ilivyotarajiwa na wengi, tulitarajia kuona kandanda safi na wangefanya vizuri zaidi kwani kama wangetulia hilo wangelifanya," alisema Tenga.

Alisema kwa sasa kinachotakiwa ni Kocha Mkuu, Jan Poulsen kufanya tathmini ya mchezo huo ili wajue jinsi gani watajipanga katika kuhakikisha wanafanya vizuri hatua ya makundi.

Tenga alisema si kwa Poulsen pekee, ila hata wachezaji wenyewe wanatakiwa wajiangalie kwanini hawakufanya kile kilichotarajiwa na Watanzania wengi na baada ya hapo anadhani watajirekebisha katika mechi zijazo.

Mbali na hilo, alizungumzia timu kwa ujumla ilivyocheza ambapo, alisema beki Kapombe alicheza vizuri sana na ana imani atafanya vizuri zaidi na hata Mrisho Ngassa na Mbwana Samatta, bado wana nafasi ya kuonesha uwezo wao zaidi.

Baada ya kufuzu kwa hatua ya makundi, Stars itachuana na Ivory Coast, Morocco na Gambia.

No comments:

Post a Comment