Na Salim Nyomolelo
SERIKALI imetakiwa kujenga mazoea ya kutoa habari kwa wananchi ili kuwawezesha kutambua mabadiriko ya sheria, maendeleo
na mipango mbalimbali ili kuepuka mkanganyiko.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana, na baadhi ya washiriki katika Mkutano wa Asasi za Kiraia (AZAKi) ulioandaliwa na Foundation for Civil Society kuwa serikali imekuwa na tabia ya kufanya siri taarifa mbalimbali huku ikifanya mabadiliko bila ya kuwashirikisha wananchi.
Akichangia hoja katika mkutano huo mmoja wa washiriki, Bw. Samson Katendale kutoka Tanga alisema kumekuwa na tabia ya watendaji wa serikali kutotoa taarifa kwa wananchi na vyombo vya habari jambo ambalo linaipumbaza jamii.
Alisema mabadiliko mengi yakiwamo ya sheria huwa yanafanyika lakini wananchi wanashindwa kujua kwa sababu ya serikali kutokuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa wananchi.
"Katiba inaeleza kuwa kuwa kila mtu anahaki ya kutoa maoni,kusambaza habari na kupewa habari bila ya kuathiri sheria nyingine za nchi," alisema
Akichangia hoja kwa upande wa vyombo vya habari katika kukuza maendeleo ya jamii, Bw. Zengo Mikomango alisema kama vyombo hivyo vikitumiwa ipasavyo vinaleta mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwa kuibua udhaifu wa watendaji, miradi na mipango mingi ambayo haitekelezeki.
Alisema pia kumekuwa na baadhi ya waandishi wa habari ambao wanatumiwa na baadhi ya vigogo kwa manufaa yake binafsi jambo ambao wanapotosha ukweli na badala yake huamriwa mambo ya kuandika.
Akifafanua hoja hizo Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Judith Ringa alisema wizara tayari imeshaandaa kituo ambacho kitakuwa kinatoa taarifa kwa jamii kuhusu mambo ya jinsia.
Alisema mchakato huo utafanyika katika Vyuo Vyote vya Maendeleo ya jamii vilivyopo mikoani ambapo zoezi hilo litaanza rasmi mwezi ujao.
No comments:
Post a Comment