Na Amina Athumani
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager leo imezindua rasmi mbio za riadha za Bendera ya Taifa ambazo ni sehemu ya Kampeni ya ‘Jivunie uTanzania’ inayoambatana na maadhimisho ya sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.
Uzinduzi huo ulifanyika jana katika makao makuu ya TBL, Dar es Salaam na kuwaleta pamoja baadhi ya wanariadha maarufu nchini watakaoshiriki katika mbio hizo zitakazofanyika mwishoni mwa mwezi huu pamoja na viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT).
Akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui alisema jumla ya wanariadha 90 watashiriki katika mbio hizo.
“Bendera zitakimbizwa na maana halisi ya rangi hizo za bendera ya Tanzania na Kutoka kanda ya Ziwa, mbio zitaanzia Mwanza ambapo Bendera ya Njano itawakilisha utajiri wa madini yetu, Kutoka kanda ya Kati, mbio zitaanzia Dodoma makao makuu ya Nchi ambapo bendera Nyeusi itawakilisha rangi yetu waafrika, na kanda ya Pwani bendera ya Bluu itawakilisha Maji,mito na vijito, wataanzia kukimbia Dar es Salaam,” alisema Nyambui.
Nyambui alisema bendera ya Kijani inayowakilisha misitu na uoto wa asili itatokea katika jiji la Arusha ambapo kila kanda itawakilishwa na wanariadha 30.
Alisema wanariadha wote watakaoshiriki wako katika hali nzuri na wamepangwa vizuri kuhakikisha kuna uwiano mzuri ili kuepusha hali ya kuwa na wanariadha wenye majina pekee katika kundi moja na wale wasio na majina.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, alisema matayarisho yote ya mbio hizo yamekamilika huku akiwapongeza wanariadha hao kwa uzalendo wao kwani kitendo hicho kina umuhimu mkubwa wakati Tanzania inaadhimisha miaka 50 ya Uhuru.
"Bia ya Kilimanjaro ina furaha kuendesha Kampeni ya Jivunie uTanzania iliyozinduliwa Julai mwaka huu a baada ya hapo kumekuwa na matamasha mbalimbali Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro na Mwanza yote yakiwa na lengo la kuwakumbusha watanzania wajivunie mafaniko waliyoyapata katika miaka 50 ya Uhuru,"alisema Kavishe.
Alisema baada ya mbio hizo wanariadha hao watakusanyika Jijini Moshi na kuipandisha bendera moja katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Kama alivyofanya Luteni Mstaafu Alex Nyirenda alipoipandisha bendera ya taifa pamoja na mwenge wa uhuru katika kilele cha mlima huo miaka 50 iliyopita.
No comments:
Post a Comment