Na Mwandishi Wetu
WAKATI vikao vya juu vya maamuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vikianza leo mjini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, hofu kubwa imetanda kuwa
huenda Kamati Kuu ya chama hicho itatoa maamuzi mazito ya kuwatimua vigogo saba wa Umoja wa Vijana wa chama hicho UVCCM.
Juzi Kamati ya Maadili iliwahoji vigogo wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa kundi linalotakiwa kujivua gamba na kutishia ustawi wa chama hicho kama wataondolewa kwa nguvu baada ya kushindwa kutii agizo la Halmashauri Kuu (NEC) la Aprili mwaka huu, ambalo liliwataka kuchukua hatua wenyewe.
Hatua ya kamati hiyo kuwahoji wafuasi, inatokana na kundi hilo kutoa kauli za chuki dhidi ya CCM na Rais Kikwete kama watawajibishwa kwa kukataa kuchukua maamuzi wenyewe.
“Kamati Kuu inatarajiwa kutoa maamuzi mazito leo au kesho kutokana na taarifa ya Kamati ya Maadili baada ya kuwahoji vigogo saba wa UVCCM na wengine,Taarifa ya maadili ni kali sana juu ya hawa watu.
“Kundi hili limetembea mikoa mbalimbali kuwarubuni wana CCM kuwaunga mkono kama mtu wao ataondolewa kwa tuhuma zinazomkabili, wewe hukusikia waliyosema Mwanza, Mara, Arusha na Iringa,ni lazima wachukuliwe hatu kali kuepusha madhara makubwa zaidi, “alisema kiongozi wa chama hicho ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa sababu sio msemaji.
Chanzo kingine ndani ya CCM kilisema, kamati hiyo ilifikia hatua hiyo baada ya kukusanya ushahidi kutoka mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Mara na Mwanza juu ya usaliti unaofanywa na kundi hilo kupitia UVCCM.
“Hawa watu wanaotakiwa kujiondoa wenyewe baada ya kupima uzito wa maamuzi ya Halmashauri Kuu iliyopita, walidhani kwamba CCM ilikuwa inacheza, baada ya kubaini watakwenda na maji wameanza kutumia njia wanazojua kukipasua CCM,” kilisema chanzo hicho.
Wakati hayo yakiendelea, kundi jingine ambalo linadaiwa kupigania na kuunga mkono maamuzi ya CCM, inadaiwa lilikuwa njiani kwenda mjini Dodoma kupambana na kundi linalotishia ustawi wa chama hicho.
“Tuko njiani, lazima watu wavue magamba kama chama kinavyotaka, hakuna kurudi nyuma,” alisema mwanachama wa kundi hilo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.
Majira lilipomtafuta Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi Bw. Nape Nnauye ili kujua maandalizi ya vikao hivyo na ukweli wa taarifa hizo, alisema kila kitu kinaendelea vizuri akikataa kuzungumzia suala la Kamati ya Maadili.
“Kimsingi mimi naweza kuzungumzia yaliyoamuliwa na NEC sio yaliyofanywa na Kamati ya Maadili, sijui chochote, ninachojua maandalizi ya Kamati Kuu na NEC yamekamilika,” alisema.
Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Wilson Mukama na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Bw. Pius Msekwa, hawakuweza kupatikana kwenye simu zao za mkononi ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo hadi tunakwenda mtamboni.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete, leo anatajia kuanza kuongoza vikao cha Kamati Kuu ya CCM mjini Dodoma ambavyo vitafanyika siku mbili na kufuatiwa na Kikao cha NEC kesho kutwa. Vikao hivyo vitatoa dira halisi ya CCM baada kutangaza mageuzi makubwa ya kujivua magamba.
Wanaochafua chama wafukuzwe
ReplyDeleteKikwete anakata tawi alilokalia mwenyewe!!Mwanzo wa Mwisho wa CCM!!!
ReplyDelete