Na Benjamin Masese, Igunga
JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora limesema vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi mdogo kwa asilimia 90 zilisababishwa na vyama vyote vya siasa
vilivyoshiriki uchaguzi huo.
Jeshi hilo limetoa tamko hilo huku viongozi wa CCM wakiendelea kutamba akuwa kuwa kilifanya kampeni za kistaarabu na vurugu katika uchaguzi huo zilikuwa zikisababishwa na CHADEMA.
"Asilimi 90 ya vurugu zilizotokea hapa (Igunga) zilisababishwa na vyama vyote vilivyoshiriki mchakato huo kwa kukodi watu kutoka mikoa mbalimbali kwa madhumuni binafsi."
Kauli hiyo ilitolewa na mjini Igunga, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia nchini (FFU), Bw. Telesphory Anaclet, ikiwa ni siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Said Mwema kueleza kuwa kwa ujumla utulivu ulitawala katika uchaguzi huo.
Bw. Anaclet alisema kuwa historia ya wananchi wa jimbo hilo inaonesha si watu wa fujo wala vurugu, bali walikuwa wanahamasishwa na wageni walioletwa na vyama vya siasa kwa malengo yao binafsi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, asilimia 10 ya wananchi wa Igunga ndio walishiriki katika maandamano na vurugu, ambapo kati ya waliokamatwa wote ni wenyeji hakuna mgeni, na inaonesha wazi walikuwa hawajui walifanyalo.
Alisema Jeshi la Polisi limewaachia kwa dhamana wafuasi wa vyama hivyo kwa uangalizi zaidi, huku likiendelea na upelelezi.
Pia jeshi hilo limeachia lori la Chadema lililokuwa limekamatwa kwa makosa mbalimbali likiwemo kupiga muziki wa kuhamasisha wananchi kuandamana.
"Kwa ujumla kitendo hiki cha vyama kukodi watu kutoka mikoa mbalimbali hakileti sura nzuri ndani ya jamii ni vema vikafanya kampeni za kistaarabu kwani siasa za uongo zinaelekea kufika kikomo," alisema na kuongeza;
"Wananchi wameelimika na wanajua pumba na mchele, huwezi kumdanganya mtu kwa nyakati hizi."
Bw. Anaclet alisema kitendo cha vyama vya kisiasa kuamini kwamba jamii fulani ndiyo inajua vurugu na fujo na kuamua kuitumia, ni kosa na ni kudharua jeshi la polisi.
Akizungumzia tathmini ya kazi yao pamoja na mchango wa waandishi alisema kuwa mbali ya kuwepo mapungufu kidogo, lakini jeshi hilo limefanikiwa vizuri kufanya kazi ya kulinda usalama wa wananchi.
Bw. Anaclet alisema mafanikio yao yanatokana na ushirikiano wa karibu na waandishi wa habari.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Tathimini na Ufuatiliaji, Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika ucjhaguzi huo, Bw. Isaya Mngulu alisema kuwa hapa nchini hakuna chama cha kistarabu, bali vyote vinafanya kampeni za kiuhuni.
Alitahadharisha wazee kukaa vizuri na vijana wa sasa vinginevyo wataipeleka nchi pabaya.
"Hakuna chama cha neema hapa, wote wahuni wanafanya mambo ya ajabu ya kukodi watu kutoka mbali kuja kufanya fujo, hawa wazee wasipokuwa makini, vijana watatupeleka pabaya," alisema.
"Binafsi sikupendezwa na kitendo cha vyama kuwaleta vijana kutoka majimbo ambayo yalikuwa na upinzani mkubwa wa kisiasa na kuwaleta hapa Igunga, hili linatakiwa kuangaliwa kwa jicho la mbali na kudhibitiwa mapema," alisema.
"Kama uchaguzi huu ungekuwa Tarime ingekuwa shughuli kubwa kusuluhisha kwa hali ile iliyojitokeza, lakini kwa watu wa hapa hawana historia ya vurugu na ndio maana wanasiasa walikodi watu kutoka huko wanakojua na sisi tulikuwa tumejiandaa vya kutosha.
Katika uchaguzi huo mgombea wa CCM, Dkt. Dalaly
Kafumu aliibuka mshindi aliyepata kura 26,484 akifuatiwa na mgombea wa Chadema Bw. Joseph Kashindye alipata kura 23,260 ambapo Bw. Leopold Mahona (CUF) aliambulia kura 2104.
Vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi huo ni AFP kilichopata kura 235, FAUSTA kura 182, DP kura 76, SAU 83 na UPDP IMEPATA KURA 63.
No comments:
Post a Comment