Na Nickson Mahundi
VIFAA vipya vya kupima chembechembe hai nyeupe zinazokinga mwili dhidi ya magonjwa (CD4) vimeingizwa rasmi nchini tayari
kusambazwa katika mikoa na wilaya zote ili kupunguza tatizo linalowakabili wagonjwa wa UKIMWI.
Akikabidhiwa mashine moja ya kupima CD4 kwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.Lucy Nkya Dar es Salaam jana, mtaalamu wa utumiaji wa vifaa vya tiba kutoka Kampuni ya Biocare Health Product Limited Bw.David Ngowi, alisema vifaa hivyo vitakuwa ni ukombozi kwa watu wa vijijini.
Bw.Ngowi alisema vifaa hivyo vinavyotambulika kwa jina la pima CD4 vitatumika kwa watu wenye elimu na wasiokuwa na elimu kwa kuwa ni vidopgo na hubebeka kiurahisi hivyo kupunguza kasi ya vifo vinavyotokana na wagonjwa wa UKIMWI kushindwa kuanza dawa mapema kwa kukosa kipimo hicho.
Alitaja faida zaidi ya kipimo hicho kuwa ni kutohitaji kuwekwa ndani ya jokofu kama vile vya zamani na vinatumia nishati ya betri yenye uwezo wa kufanya kazi zaidi ya masaa nane ambayo itakuwa ni rahisi kutumika na watoa huduma majumbani maeneo ya vijijini.
"Kifaa hiki kitawasaidia wagonjwa wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI wasiokuwa na fedha za kufika katika hospitali kubwa kupimwa wakiwa majumbani mwao hasa vijijini,",alisema Bw.Ngowi.
Akipokea kifaa hicho licha ya kutoa shukrani pia Dkt.Nkya aliahidi kuwa serikali kupitia wizara yake itahakikisha usambazaji wa vifaa hivyo kuanzia ngazi ya vijiji,wilaya na Mikoa unafanyika haraka iwezekanavyo ili tatizo la kipima CD4 liweze kupungua vijijini.
Alishauri taasisi zinazojishughurisha na huduma kwa wagonjwa wa UKIMWI kutumia fursa hiyo katika bajeti zao kuisaidia serikali katika usambazaji pamoja na elimu ya jinsi ya kuvitumia.
"Kifaa nilichokipata nitakipeleka kijijini kwangu na nitaikabidhi Serikali ya Kijiji kwakuwa wana wahudumu wa wagonjwa majumbani itakuwa ni vema kama watawatumia hao kuwapima wenye upungufu wa DC4,"alisema Dkt Nkya.
Bw.Ngowi aliwataka wananchi watakaopata vifa hivyo kuvimiliki na kuacha urasimu katika matumizi wawapo vijijini hasa kwa familia masikini.
No comments:
Post a Comment