12 October 2011

Maiti ya wakala CHADEMA yaokotwa Igunga

Na Mwandishi Wetu

MAITI ya kada na wakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyepotea wakati wa uchaguzi wa Igunga imeokotwa katika pori la Magereza
ikiwa imeharibika vibaya.

Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, Marehemu Masoud alikuwa ni mmoja wa wanachama walijitolea kusafiri kwenda Igunga kuwa wakala kwenye uchaguzi Oktoba 2, 2011 na alitoweka katika mazingira ya kutatanisha wilayani Igunga Septemba 30, 2011.

Baada ya jitihada za viongozi wa chama kumtafuta kushindikana Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Kinondoni ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bw. John Mnyika alitoa taarifa polisi Oktoba 3, 2011 na kufungua jalada RB/748/2011.

Tangu wakati huo, kijana huyo hakuonekana tena hadi Oktoba 9, 2011 baada ya wananchi wilayani Igunga kukuta mwili wa marehemu ukiwa porini katika eneo ambalo linajulikana kama Msitu wa Magereza.

Taarifa ilitolewa na wananchi kwa diwani wa Kata ya Igunga, Bw. Vicent Kamanga (CHADEMA) ambaye alifika katika eneo hilo na baadaye maofisa wa polisi walifika na kupeleka mwili huo katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Baadaye siku hiyo, Bw. Mnyika alitembelea nyumbani kwa marehemu katika Mtaa wa Kwa Jongo, Kata ya Makurumla jijini Dar es Salaam kuifariji familia ya marehemu na kukubaliana na ndugu wa marehemu kutuma wawakilishi kuambana na wengine wa chama kwenda Igunga kuhakiki mwili uliopatikana.

Juzi, wawakilishi wa familia wakiwa pamoja na Katibu Mwenezi wa Chama Wilaya ya Ubungo, Bw. Ali Makwilo walishuhudia mwili husika na kuthibitisha kuwa ni wa marehemu Mbwana Masoud.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa kidaktari (post mortem) jana na kubaini chanzo cha kifo na ripoti wamepatiwa jeshi la polisi.

Hata hivyo, chama hicho kimesema mazingira ya kupatikana kwa mwili wa marehemu yanaashiria Masoud aliuawa na maziko yake yalitarajiwa kufanyika jana alasiri katika Kata ya Igunga yakihusisha wawakilishi wa familia ya marehemu, viongozi wa chama, wanachama na wananchi wa maeneo husika.

Mbowe alaani mauaji

Taarifa iliyotolewa baadaye Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Bw. Freeman Mbowe ilisema taarifa za uchunguzi wa awali zinaonesha kuwa, Bw. Masoud alikuwa na majereha, macho kutobolewa, kichwa kupasuliwa kutokana na kipigo pamoja na kumwagiwa tindikali ambayo ilibadilisha taswira yake,” alisema Bw. Mbowe.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kinavitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi haraka na kuwakamata wote waliohusika na unyama huo pia wanatoa wito kwa mwananchi yeyote anayetambua chochote kuhusu kifo hicho, atoe taarifa kwa vyombo vya usalama na CHADEMA kwa ufuatiliaji zaidi.

Bw. Mbowe alisema kutokana na mwili huo kuharibika vibaya na chama hicho kushauriana na ndugu wa marehemu, wamekubaliana azikwe Igunga jana saa saba mchana kwa heshima zote za chama, ambapo kesho, kutafanyika maombi Jijini Dar es Salaam.

1 comment:

  1. Mh! kwa mwendo huu, tutafikishana pabaya! Rwanda ilianza hivi hivi

    ReplyDelete