Na Faida Muyomba, Geita
MTU mmoja ameuawa kwa risasi na wangine wanne wakiwemo askari polisi watatu kujeruhiwa, katika mapambano ya polisi na wachimbaji wadogo wa dhahabu katika
Kijiji cha Nyarugusu, wilayani Geita, baada ya wachimbaji hao kuvamia eneo la mgodi uliofungwa wakitaka kuchimba madini hayo.
Akithibitisha kuwepo kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Bw. Liberatus Barlow alimtaja aliyeuawa katika tukio hilo lililotokea jana saa tatu asubuhi kuwa ni Bw. Jahaja (26) ambaye alipigwa risasi na polisi kichwani na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita.
"Ni kweli mtu mmoja ameuawa kwa risasi na watu wanne akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyarugusu, Bw. Ibrahim Mbulu wamejeruhiwa. OCS amejeruhiwa mkono wake wa kushoto, na askari wengine wawili na raia mmoja, Bw. Heneriko yeye alijeruhiwa kwa risasi katika mguu wake wa kushoto," alisema Kamanda huyo wa polisi.
Alisema gari la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (Mwanza) lenye namba za usajili PT 1499 na magari mengine mawili ya raia yenye namba T 712 AUJ na T.628 BQQ yalivunjwa vioo kwa kupigwa mawe na wananchi hao ambao walitaka kuteka Kituo cha Polisi cha Nyarugusu.
Alisema kutokana na hali hiyo, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi, riasi za plastiki lakini walionekana kuzidiwa na wananchi hao na ndipo walitumia riasi za moto kuwatawanya wakiwa wamekaribia kituoni hapo.
Kamanda huyo alisema pia watu hao walianza kuvunja nyumba ya Bw. Baraka Nyandu na nyingine ya Evarini Evaristi ambazo zilivunjwa vioo vyake huku baadhi wakiwa wameanza kuwasha moto kwa kutumia petroli kwa madai kuwa ndio chanzo cha mgodi huo kufungwa.
Wakizungumza na waandishi habari katika eneo la tukio, baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, walisema lilidumu kwa muda wa saa tano ambapo wananchi walitumia mawe kuwarushiwa polisi na polisi wakitumia mabomu ya machozi na risasi kuwatawanya.
Vurugu hizo zinadaiwa kutokea katika mgodi wa dhahabu ulioko Kijiji cha Nyaruyeye ambao ulifungwa na serikali lakini wao walilazimisha ufunguliwe kwa madai kuwa kuna dhahabu nyingine lakini wakakutana na nguvu ya polisi, hivyo kushindwa kuingia eneo hilo.
Baadaye watu hao walianza kukusanyika na kufanya maandamano huku wakiichoma bendera ya CCM na kutundika ya CHADEMA, kisha kuzunguka mitaani kwa maandamano huku polisi wakiwazuia.
No comments:
Post a Comment