Heckton Chuwa na Flora Temba, Moshi
WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Cleopa Msuya, amesema serikali haikulifuta Azimio la Arusha na kubadilishana na lile la Zanzibar, bali hayo ni mawazo ya wachache waliokuwa na
tamaa ya kunyakua mali ya umma.
Bw. Msuya alitoa kauli hiyo juzi wakati wa mahafali ya kumi ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari ya Mt. Maria Goreti ya mjini Moshi, mkoani Kilimanjarokwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na kusisitiza kuwa, siasa ya Tanzania bado ni ya Ujamaa na Kujitegemea.
“Mimi nilikuwa kwenye kile kikao cha Zanzibar, tulichokubaliana kuwa kulingana na mabadiliko yaliyokuwepo wakati huo, mtu akiweza kujiingizia kipato kwa njia ya halali afanye hivyo ili mradi azingatie maadili mema na sio kuliua Azimio la Arusha”, alisema.
Alisema lengo lilikuwa ni kupotosha wale waliokuwa na tafsiri mbaya kuhusu Azimio la Arusha kwa kuwa ilifikia wakati mtu akifuga kuku ishirini, thelatini au hata mia moja ni sawa lakini akiwa na kuku zaidi ya mia mbili tena wa halali anaitwa kabaila jambo ambali alisema ilikuwa ni tafsri potofu ya Azimio la Arusha.
“Lakini wachache wenye uchu wa kunyakua mali ya umma wakaanza kufanya hivyo kwa kisingizio cha kikao kile cha Zanzibar huku wakitafsiri maazimio ya kikao kile visivyo ili kuhalalisha tamaa zao”, alisema.
Aliongeza: “Wananchi watashinda vita dhidi ya ufisadi kuwa bado wanalitaka Azimio la Arusha na ndio maana mnaona kwenye vyombo vya habari kila siku watu wakipambana na wavamizi wa ardhi na mali nyingine za umma”.
Kuhusu dhana kuwa Watanzania wanaogopa Shirikisho la Afrika Mashariki, Bw. Msuya alisema dhana hiyo si kweli na kwamba ukweli ni kwamba watanzania wanafuatilia suala hilo kwa umakini kutokana na hadhi na heshima ya Tanzania kimataifa.
“Sisi hatuogopi shirikisho bali tunachukua tahadhari na umakini mkubwa, lengo letu ni kuwa maamuzi yetu yasije kutuunganisha na matatizo ya wengine”, alisema.
Alisema kuwa kuna baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao bado hali zao kiusalama bado si nzuri na ndio sababu ya hadhari ya Tanzania na kwamba si vyema Tanzania ikaacha utaifa wake na kujiunga shirikisho bila ya kuwa na hadhari juu ya hali yake ya baadaye.
“Ushauri wangu ni kwamba tuimarishe eneo la biashara kwanza miongoni mwa mataifa yetu ya Afrika Mashariki na ndipo tufikirie ushirikiano wa kisiasa”, alisema.
Si manyangau hiyo mijitu. Ona yanakotupeleka
ReplyDelete