Na Tumaini Makene
RAIS JAKAYA Kikwete jana alitumia hotuba yake katika Baraza la Siku Kuu ya Eid El-Fitr, kuelezea na kusisitiza msimamo wa serikali katika masuala kadhaa yanayohusu
mstakabali wa taifa, hususan yale ambayo yamekuwa yakizua mijadala mikubwa nchini, yakichukua milengo ya imani za dini, kama vile suala la Mahakama ya Kadhi, dhana ya udini nchini na katiba mpya.
Kwa mara ya kwanza, Rais Kikwete amezungumzia kwa undani juu ya mchakato wa uundwaji wa Mahakama ya Kadhi, akisema kuwa serikali haitahusika katika uendeshaji wake, lakini akatoa rai kuwa, imelazimika kuhusika katika uanzishwaji wake, ili kuhakikisha kuwa kitakachoundwa hakiendi nje ya masuala ya dini, akisema kuwa mahakama hiyo haitahusika kuhukumu jinai, wala kutoa adhabu za kukata watu mikono.
Rais Kikwete pia alikumbushia wito wake kwa dini zote kuwa, midahalo juu ya katiba mpya, isitumiwe kama jukwaa la malumbano ya waislamu na wakristo, kila mmoja akitaka kuingiza maslahi ya dini yake katika katiba, akisema kuwa suala hilo linaweza kuchelewesha upatikanaji wa mwafaka huo wa kitaifa na hata kuibua ya uvunjifu wa amani iliyopo, akisema katiba mpya inapaswa kuwanufaisha watu wote, bila kujali tofauti mbalimbali kama vile dini.
Katika hotuba hiyo ya dakika 65 mbele ya umati uliohudhuria Baraza la Eid, lililofanyika jana katika Msikiti wa Ghaddaf, mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema wazi kuwa serikali haina mpango wa kurejesha shule zilizokuwa zikimilikiwa na madhehebu mbalimbali ya dini, kabla hazijataifishwa na serikali ya awamu ya kwanza, akiyataka sasa yajikite katika ujenzi wa shule zingine mpya, badala ya kudai hizo za zamani, akiahidi kuwa hazitataifishwa tena.
Suala jingine ambalo Rais Kikwete alilizungumzia ni malalamiko ya muda mrefu ya baadhi ya watu nchini juu ya kuwepo kwa Makubaliano Rasmi (MoU) kati ya serikali na baadhi ya makanisa ya Kipentekoste na Kanisa Katoliki, ambapo serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwa makanisa hayo au mashirika yaliyo chini yake katika shughuli za kijamii yanayofanya, kama vile kutoa elimu na matibabu, sehemu mbalimbali nchi nzima.
Akitumia sehemu ya hotuba yake hiyo kujibu risala ya waumini wa Kiislamu, ambao kupitia kwa Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), walisema kuwa serikali imekuwa ikilegalega katika nia ya kurejesha mahakama ya kadhi nchini na pia kushughulikia dhana ya udini, Rais Kikwete alisisitiza msimamo wa serikali kuwa haitakuwa na dini rasmi ya taifa, bali watu wake, mmoja mmoja au kundi, watakuwa na uhuru wa kuabudu au kutokuabudu.
"Mliyosema katika risala yenu, nimeyasikia na kuyaelewa na tutayazingatia. Maneno haya nitakayoyasema si mageni kwenu. Nimeshasema mara kadhaa. Serikali inatambua sana nafasi ya dini na mashirika ya dini katika ustawi wa jamii ya Watanzania. Na ndiyo maana ya itifaki hiyo ya makanisa na serikali mliyoisema, kwa sababu serikali inatambua manufaa yake katika kuwapatia Watanzania huduma kama vile afya na elimu.
"Bila ushirikiano huo wa serikali na makanisa, upatikanaji wa huduma hizo katika baadhi ya maeneo ungekuwa tofauti sana, ama ungedorora au usingekuwepo kabisa, hivyo serikali inasaidia ili kufanikisha huduma hizo. Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna chochote kitatolewa kwa dini yoyote ile ambacho kitanyimwa kwa dini nyingine ambayo inastahili kupata. Kwa serikali dini zote ni sawa.
"Kama hujaomba usilaumu. Usilalamike mwenzio akiomba na kupata, wakati wewe hujaomba, kama sifa unazo omba. Ukifanyiwa vinginevyo udai haki yako katika mamlaka husika. Nimesikia kuwa na nyie mmeamua kuleta maombi yenu, nasema mmechelewa, tangu mwaka 1992 mnalalamika tu bila kuomba, leteni maombi yenu yatafanyiwa kazi.
Katika kutatua suala la dhana ya udini, ambalo limekuwa likidaiwa kuwa lilidhihirika katika uchaguzi mkuu uliopita, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini, kurejesha utataribu wao wa zamani wa kukutana kujadili masuala anuai, akisema 'wanaozungumza hawagombani, lakini wasiozungumza hugombana', akisema kuwa nguvu ya dola haiwezi kuwa jawabu katika hilo.
"Na hili ni kwa viongozi wa dini zote, hivi kwani hamuwezi kueneza dini zenu bila kukashfu au kubeza dini za wenzenu, acheni hayo, ndiyo maana uhuru wa kuabudu unalindwa kisheria, kila mtu anao uhuru wa kuabudu na wengine hawaamini kabisa na si vizuri kuwalazimisha. Na sasa ni vyema mkafufua ule utaratibu wa zamani wa viongozi wa dini kukutana. Yazungumzeni yanayoisibu nchi. Kwa ushahidi huko mtakubaliana kuwa katika hili mlikuwa katika mstari mbaya," alisema Rais Kikwete na kuongeza;
Mapema akisoma risala, Katibu Mkuu wa BAKWATA, aliitaka serikali kuwataja kwa majina viongozi wa dini ambao wamekuwa wakisemekana kuwa wanajihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, badala ya kutoa shutuma za jumla jumla, huku akisema kuwa baraza hilo liko ayari kutoa ushirikiano kwa serikali katika suala hilo.
Z'BAR KUAJIRI 2,476
Na Mwajuma Juma, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amesema Serikali inatarajia kuajiri watu 2,476 mwaka huu wa fedha katika kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa wananchi wake.
Alisema hayo jana wakati akihutubia Baraza la Iddi lililofanyika katika ukumbi wa Bwawani kufuatia kukamilika kwa Mfungo wa Mwezi wa Ramadhan iliyoanza Agosti Mosi mwaka huu.
“Serikali inatarajia kuajiri watu hao kulingana na mahitaji na uwezo uliopo ili kukabiliana na uhaba wa fursa za ajira”, alisema Dk. Shein.
Hata hivyo aliwataka wananchi kujiunga na vikundi vya ushirika ili wanufaike na mpango endelevu wa kusaidia vikundi vya uzalishaji mali kwa lengo la kujiajiri na kufanikisha mpango wa kukuza Uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi wake.
Kuhusu kilimo alisema Serikali imeamua kuziimarisha shughuli za kilimo kwa kupunguza bei za pembejeo na huduma za matrekta kuanzia mwaka huu wa fedha.
Alisema katika kutekeleza mpango wa mapinduzi ya kilimo maandalizi yameanza ya kuajiri wataalamu wa kilimo wakiwemo mabibi na mabwana shamba na kuimarisha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.
Alisema lengo ni kuongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa wananchi kupitia sekta hiyo pamoja na sekta ya uvuvi na ufugaji. Hata hivyo aliwataka wakulima wa zao la karafuu kujiepusha na biashara ya magendo ya karafuu kwa vile biashara hiyo haina manufaa kwa wakulima na Serikali.
Aidha amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuimarisha usalama hasa wa barabarani katika kipindi chote cha Mfungo wa Ramadhan na kuwatakia maofisa wa Polisi wa Usalama barabarani wawe makini kusimamia vizuri sheria hiyo ili kuepusha ajali katika kipindi hiki cha sikukuu.
Dkt. Shein aliwashukuru wananchi wote wasiokua waumini wa kiislamu kwa kuonesha ushirikiano wa dhati katika kipindi chote vcha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
KAULI YA GHARIB BILAL
Wakati huo huo, Makamau wa Rais Dk. Mohamed
Gharib Bilal ameitaka jamii kuungana kwa pamoja katika kuhimiza maadili mema na kukemea maovu badala ya jukumu hilo kuwaachia viongozi wa dini peke yao.
Akizungumza katika sala ya Idd El Fitri iliyoswaliwa kimkoa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dkt. Bilal alisema jamii isiwategemee viongozi wa dini katika kupambana na maovu yanayoendelea kukithiri ndani ya jamii.
Dkt. Bilal alisema kila mwanajamii kwa upande wake anatakiwa si kuacha bali pia kukataza mambo yote mabaya. “Haitoshi kwa muumini mmoja kuwa mwema peke yake, halafu akayafumbia macho maovu yanayotokea katika jamii inayomzunguka,” alisema Dkt Bilal.
Kwa mujibu wa Dkt. Bilal alisema Watanzania hawana budi kuona fahari pia kuyatekeleza maelekezo ya mwenyezi Mungu ya kuifanya Dunia yote kuwa yenye neema, kwa kuwa umahiri ameutukuza Mwenyezi Mungu kuwa umma bora.
Dkt. Bilal pia aliwashukuru waumini wa dini nyingine kwa ushirikiano wao wa dhati kwa ndugu zao waislamu, ulioweka mazingira mazuri katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa upande mwingine Dkt. Bilal pia aliwataka waislamu nchini kuendelea kufanyiana mema ikiwemo kutoa sadaka, kuswali na kufanya ibada pamoja na kuwasaidia wasiojiweza mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha mfungo.
Akifafanua zaidi alisema si imani safi kudhani kuwa mema yanapaswa kutendeka tu wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na badala ya hapo kuanza kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili.
“Napenda kuwaasa ndugu zangu waislamu kuzingatia wajibu wetu kama waumini, kufanya mambo mema na kuyaacha yote mabaya kama tunavyoamrishwa” alisema Dkt. Bilal.
No comments:
Post a Comment