22 September 2011

Polisi, wizara, waanza kudhibiti sukari

Anneth Kagenda na Rachel Balama

SIKU moja baada ya Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kutishia kutumia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuzuia  magendo ya sukari, Jeshi la
Polisi limezinduka na kutangaza operesheni ya wiki mbili kwa ajili ya kuwanasa wafanyabiashara wote nchini wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Jeshi hilo limewaagiza Makamanda wa Polisi nchini kuhakikisha askari wote wanaojihusisha na vitendo vya kusindikiza wafanyabiashara wa magendo ya sukari wanashughulikiwa ipasavyo.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), Kamishna Robert Manumba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Polisi kuhusu operesheni ya jeshi hilo dhidi ya wanaojihusisha na kusafirisha, kuhodhi na kuuza sukari au mahindi kwa bei ya juu.

Alisema kuwa operesheni hiyo ya nguvu iliyoanza juzi  itadumu kwa wiki mbili nchi mzima ambapo watafanya ukaguzi katika magodauni, maeneo ya wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo na wote watakaobainika kuhodhi, kuficha, kuuza bei ghali, kusafirisha nje ya nchi kwa makusudi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema kuwa vitendo vya kusafirisha, kuhodhi na kuuza sukari au mahindi kwa bei ya juu haviwezi kufumbiwa macho na yeyote atakayebainika akijihusisha na vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufunguliwa mashtaka na kufikishwa mahakamani.

"Jambo kubwa lililopo mbele yetu ni wimbi la kuongezeka kwa uhaba wa sukari hapa nchini, ambapo utafiti umeonyesha kuwa uhaba huo umesababishwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kuhodhi bidhaa hiyo ili kusababisha upungufu sokoni," alisema na kuongeza;

"Utafiti pia umeonyesha kuzuka kwa soko la bidhaa hiyo kwenye nchi jirani, hivyo wafanyabiashara wasio waaminifu kwa kuvutiwa na bei kubwa katika masoko hayo kuanza kuvusha sukari kinyume cha sheria na kwenda kuiuza nchi za jirani," alisema Bw. Manumba.

Alisema jeshi la polisi nchini kwa kushirikiana na Taasisi zingine kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Sukari, Uhamiaji, Wizara ya Biashara, Shirika la Viwango Nchini (TBS), Bodi ya Ushindani, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na Usalama wa raifa (TISS) limeandaa operesheni maalumu ili kuhakikisha kwamba sukari inapatikana kwa kiwango cha kuridhisha katika soko la ndani na kwa bei elekezi iliyokubaliwa na wadau wote husika.

Aidha aliwaonya wafanyabiashara wote wanaojihusisha na kuficha, kusafirisha sukari nje ya nchi kinyume cha sheria au kuuza sukari hiyo kinyume na bei elekezi waliyokubaliana kuacha tabia hiyo mara moja na yeyote atakayekaidi na kuendelea kufanya uhalifu huo atakamatwa na hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.

Akijibu maswali ya waandishi moja wapo likiwa ni lile lililohoji kuwa ni kwanini wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya Bw. Pinda kuonekana kukosa imani na jeshi hilo, alisema kuwa ukweli ni kwamba jeshi lipo kwa ajili ya kupokea taarifa kutoka sehemu yoyote hivyo ni jambo la busara kupata taarifa hiyo na wao ndio wanaanza kulifanyia kazi kwa hali na mali ili kuwabaini wahusika.

Kauli hiyo imekuja baada ya Waziri Pinda kulipa muda Jeshi hilo na kutangaza kuwa ikiwa vitendo hivyo vitaendelea basi ataitumia JWTZ kuchukua hatamu.

Wizara hayo yanena

Naye Edmund Mihale anaripoti kuwa serikali imetangaza hatua tatu za kuchukuwa ili kukabiliana na hali mbaya ya uhaba wa sukari nchini unaosababisha bei kupanda ikiwemo kutoa onyo kwa wafanyakabishara watakaobainikia kukiuka hatua hizo kufutiwa leseni.

Akizungumuza na waandishi wa habari jana Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Ushirika, Bw Geofrey Kirenga, aliasema kuwa hatua hizo ni kuruhusu ununuzi wa tani 120,000 kutoka nje kuingia soko la ndani ambayo itafutiwa ushuru wa forodha ili bei yake ilingane na ile ya inayozalishwa ndani ya nchi.

Pia serikali itafuatilia kwa karibu uzalishaji na usambazaji wa sukari kutoka viwandani hadi ngazi ya wilaya na kuanzia sasa kila kiwanda kinatakiwa kuwasilisha katika Bodi ya Sukari uzalishaji wake wa kila siku.

Hatua nyingine ni kutoa taarifa za kila mnunuzi, jina la kampuni namba ya simu ya mkononi ya mwenye kampuni hiyo na kiasi alichouziwa kwa siku hiyo. Namba za magari yaliyopakia sukari, mwenye gari, wilaya atakayosambaza sukari hiyo na tarehe atakayofika wilayani.

Alisema kuwa Makatibu Tawala wa Wilaya zote wanatakiwa kupeleka taarifa hizo wizarani kila siku kuhusu sukari iliyoingia kiasi, imenunuliwa kutoka kampuni gani (pamoja na vielelezo ikijumuisha namba ya gari na simu ya mwenye gari).

Alisema kuwa wasambazaji wa sukari kutoka viwandani wanatakiwa kupeleka Bodi ya Sukari kila siku kiasi cha sukari walichopokea kutoka kiwandani pamoja na jina la kiwanda na nani aliuziwa namba ya simu ya kiongozi mkuu wa kampuni, kiasi alichouziwa na ataisambaza sukari wilaya gani na atafika wilayani lini.

"Mfanyabiashara yeyote atakayekiuka utaratibu huu au kushindwa kutoa  taarifa sahihi atafutiwa leseni yake mara moja," alisema Bw. Kirega.

Naye Gift Mongi, anaripoti kutoka Moshi kuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labaur Party (TLP) Bw. Augustino Mrema, amelitaka Jeshi la polisi nchini kufanya kazi zake kwa uadilifu na ufanisi zaidi na kama tayari linaonaekana kushindwa kazi ya kulinda mipaka ya nchi, basi kazi hiyo iachwe kwa JWTZ.

Bw. Mrema alitoa kauli hiyo wakati akikagua eneo ambalo majambazi yalipora na kusababisha kifo cha mfanyabiashara mmoja na kujeruhi watu wengine wawili.

Bw. Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (ALAAT) alisema polisi kwa sasa si waadilifu kama ilivyokuwa zamani.

“Yaani polisi anasikia mlio wa bunduki ya jambazi anavamia, lakini
badala ya kwenda eneo la tukio anang'ang'ania kusindikiza mahindi
yanayovushwa kwenda nchi jirani za Kenya, hii ndio kazi yao
kweli?" alihoji, Bw. Mrema ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

1 comment:

  1. Polisi gani wakati wao ndio wanaosindikiza magari ya kuvusha sukari kwenda nchi nyingine? Inajulikana siku zote kwamba jeshi la polisi limeoza kwa rushwa na ufisadi. Misingi ya ujambazi katika jeshi uliojengwa katika awamu ya tatu unaendelea na sasa tunauona katika kila aina ya ujambazi: kwenye mabenki, kwa vijana wafanya biashara ya mawe, kubambikia watu makisi, kusababisha ajali mbaya za barabarani, kusindikiza magari yanayofanya magendo mipakani, kutesa watuhumiwa wasiokuwa na hatia, n.k. Polisi ni laana tupu. Polisi ni tishio kwa wananchi.

    ReplyDelete