Na Mwandishi Wetu
MFANYABIASHARA maarufu wa Zanzibar, Bw. Mohamed Raza amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuwashinikiza makada na baadhi ya viongozi wake
wenye tuhuma mbalimbali za ufisadi kujiondoa ili kufanikisha falsafa ya kujivua gamba.
Pia mfanyabiashara huyo ameonya kuwa endepo hatua hiyo iliyoanzishwa na Halmashauri Kuu wa Taifa ya chama hicho haitatekelezwa kwa ukamilifu hali hiyo itakiumiza chama hicho.
Bw. Raza aliyewahi kuwa Mshauri wa Rais wa Zanziibar wa masuala ya michezo, alisema hayo jana alipotembelea ofisi za gazeti hili na kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu chama hicho, serikali na hatima ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Kuhusu kujivua gamba, viongozi tuwe wakweli. Kila anayetuhumiwa kwa ufisadi ajiondoe, hapa hakuna nafasi ya mahakama," alisema.
Alipoulizwa ni akina nani wanaotakiwa kujiondoa, Bw. Raza alisema: "Wako wengi ndani ya chama na wanajijua, maana wanatajwa kila siku na magazeti wanayasoma. Wajiondoe au waondolewe, huo ndio ustaraabu," alisema.
Alisema watuhumiwa hao wanatakiwa kutambua kuwa wao si maarufu kuliko chama. "Umaarufu ni wa chama sio wa mtu. Ndani ya chama hakuna bwana, wakiache chama kiendelee."
Kuhusu tume za rais
Bw. Raza aligusia wingi wa tume zinazoundwa na marais wa muungano na wa Zanzibar akidokeza kuwa matokeo yake hayafanyiwi kazi licha ya kutumia zaidi ya sh bilioni 10 za walipa kodi tangu uhuru.
Kutokana na hali hiyo, Bw. Raza alipendekeza katika kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika ripoti za tume hizo ziwekwe wazi ili wananchi wazisome na kujua kilichomo.
"Imekuwa kiongozi anaunda tume, inaleta taarifa, akifungua anakuta yumo ndugu wake, yumo jamaa yake, yumo swaiba wake anaamua kuachana nayo na kuifungia. Watumishi wamekuwa si waaminifu, urafiki wao, undugu wao na uswahiba wao unaididimiza nchi," alisema.
Kauli ya Muungano
Akizungumzia muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Bw. Raza alisema wakati mjadala wa Katiba Mpya unaendelea, Wazanzibar waruhusiwe kwenda kama nchi kupeleka hoja zao sambamba na zile za Serikali ya Muungano ili kumaliza kile alichosema ni kero za zaidi ya miaka 40.
"Tusilazimishane, tuheshimiane na kama watendaji waliopewa kazi hii wameshindwa wajiuzulu," alisema Bw. Raza huku akiomba Rais Jakaya Kikwete amteue kuwa mbunge kwa mwezi mmoja (bila mshahara wala posho) ili aongoze Wazanzibari wakati wa mjadala wa katiba mpya kwa maslahi ya nchi yake.
Alisema kipindi hiki cha mjadala wa katiba ni muhimu kwa Zanzibar kuhakikisha kero za muungano zinamalizwa vinginevyo fursa hiyo ikipotea hawataipata tena.
Ana wazimu, epewe Ubunge na nani? wnanchi hawamtaki, Mkwajuni hakuambulia kura hata moja ya maoni, urais ndio kabisaaaa wa tiro, bado tu anaota vyeo! Ama Salimini alimroga vibaya! kesha, gendaheka!
ReplyDelete