Na Waandishi Wetu
JESHI la Polisi limebomoa nyumba 62 eneo la Kunduchi Mtongani kwa kile kilichodaiwa kuwa zimejengwa eneo la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ).Ubomoaji wa
nyumba hizo umeripotiwa kuanza jana alfajili saa 11 na kusababisha wananchi kushindwa kuokoa mali zao.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya mashuhuda walidai ubomoaji wa nyumba hizo umefanyika ghafla na kuelekeza lawama kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Jordan Rugimbana, wakidai ndiye aliyesababisha nyumba zao zinabomolewa.
Mashuhuda walisema ubomoaji wa nyumba hizo ulisimamiwa na Kikosi cha Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa na mabomu ya machozi, silaha za moto na magari ya maji ya kuwasha.
Uboaji wa nyumba hizo ulisimamiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela. Akizungunza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Bw. Kenyela alikiri kusimamia operesheni hiyo.
Hata hivyo alitofautiana na wananchi kuwa vilivyobomolewa ni vibanda 24 na si nyumba kama inavyodaiwa.
Alifafanua kuwa hatua hiyo ilikuwa ni utekelezaji wa amri iliyotolewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Dar es Salaam na ile ya polisi kuwa vimejengwa eneo la Jeshi JWTZ na kwamba wananchi hao walikuwa wamebakiza mita 50 kuingia sehemu zinapohifadhiwa silaha za jeshi.
Bw. Kenyela alisema eneo hilo halikuwa makazi tu, bali wananchi wao wameliharibu kwa kuchimba mchanga na kokoto.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kawe, Bi. Halima Mdee alionesha kushangazwa na usiri wa bomoa bomoa hiyo waliofanyiwa 'watu wake' bila viongozi wa wananchi, kwa maana ya mbunge na diwani wa kata husika kutaarifiwa.
Alisema hali hiyo inadhihirisha kuwa hatua hiyo haikuwa na nia njema na imefanywa kwa malengo ya kisiasa zaidi.
Akizungumza kwa simu akiwa Igunga, mkoani Tabora, Bi. Mdee alisema kuwa alipata taarifa za wananchi wa jimboni kwake kubomolewa nyumba zao jana asubuhi, kisha akachukua hatua ya kumpigia simu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi, ambaye naye, kwa mujibu wa mbunge huyo, hakuwa na taarifa.
Pamoja na ofisi yake kulifanyia kazi suala hilo tangu jana asubuhi baada ya kupata taarifa, Bi. Mdee alisema kuwa atakaporejea kutoka Igunga, atalivalia njuga ili kubaini hatua zinazostahili kuchukuliwa, ikiwemo za kisheria ikibidi, ili kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake iwapo serikali itakuwa imekiuka haki za wananchi waliobomolewa.
No comments:
Post a Comment