02 September 2011

Luhanjo atumiwa kukaidi amri ya Mahakama Kuu

Na Mwandishi Wetu

UONGOZI wa Chama cha Muungano wa vyama vya wakulima wa chai Lupembe (MUVYULU) chini ya katibu wake Bw. Medeck Mhomisoli unatumia wadhifa wa
Katibu Mkuu kiongozi Bw.Philemon Luhanjo kupuuza amri ya Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi, kwa kuendelea kuvuna magogo katika Msitu wa Iyembela ulioko Njombe uliozuiwa na mahakama hiyo.

Mahakama Kuu ilitoa amri Agosti 22 mwaka 2008 kwa chama cha MUVYULU kutojihusisha na msitu huo pia kuondolewa kwa watu waliovamia kiwanda cha chai cha Lupembe ambacho kilibinafsishwa pamoja na msitu huo.

Kufuatia amri hiyo iliyotokana na kesi ya msingi na.193 ya mwaka 2008, katibu wa chama cha MUVYULU aliandika barua Januari 31 mwaka huu akimwomba Bw.Philimon Luhanjo kuvuna magogo ya msitu huo hata kama umezuiwa na mahakama  na kumuomba aviarifu vyombo vya usalama kumpa ulinzi asibughudhiwe na yeyote.

Katika barua hiyo ambayo Majira imeiona, katibu wa MUVYULU anawataja wajumbe wa Bodi ya MUVYULU waliokaa na kupitisha uamuzi wa kupingana na mahakama kuwa ni Sylvesta A.Kabelege (Mwenyekiti), wajumbe ni Augostino S.Hongole, Wilbert  Pelekamoyo, Jochindus Mgodamkali na Andrew M.Ulungi ambao walikaa kikao hicho Agosti 24 mwaka jana.

Kikao chao kilikuwa na ajenda nne,ambazo ni kufungua mkutano, uuzaji wa magogo ya nguzo za umeme kutoka msitu wa Iyembela (uliozuiwa na mahakama). Mengineyo na kufunga mkutano na wajumbe wote kuweka sahihi zao katika mhutasari wa kikao hicho.

Baada ya kupewa baraka na Katibu Mkuu Kiongozi, walianza kuvuna na Julai 26 polisi walikamata watu wawili kwa kosa la kuvuna msitu wenye kesi mahakamani, lakini polisi Njombe walidai kuzuiwa na kile walichoita mamlaka za juu wasiwafikishe mahakamani watuhumiwa.

Agosti 3, mwaka huu waandishi wa habari wa gazeti hili baada ya kumkosa IGP Said Mwema aliyedai yupo msibani, walikwenda kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Bw.Robert Manumba na kuhojiana naye kuhusu polisi Njombe kushindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria naye aliomba muda kufuatilia suala hilo na kuahidi kuwajulisha waandishi wetu alichochunguza.

Hata hivyo imefikia mwezi sasa amekuwa hapokei simu wala yeye kupiga kueleza alichochunguza, na kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Shamsi Vuai Nahodha alipokutana na mmoja wa waandishi wetu aliomba kupatiwa nakala ya amri ya mahakama ili kujiridhisha na akibaini kuna uzembe wa askari polisi atachukua hatua.

“Polisi hawezi kujitetea kuwa hakutekeleza sheria kwa sababu alitumwa na Katibu Mkuu Kiongozi au hata nani…je siku mambo yakiwa mabaya atamwita aliyemtuma asitekeleze sheria  amtetee? Mimi nitafuatilia kuona kama kuna mamlaka nyingine inayozuia utekelezwaji wa sheria,” alisema Waziri Nahodha.

Mwishoni mwa wiki iliyopita malori mawili moja likiwa na namba za usajili T207 AAG na lingine likiwa na namba za serikali SU 32338 yote aina ya Scania yalionekana kusomba magogo ya nguzo kutoka katika msitu huo na kupeleka kusikojulikana.

Mwaka jana wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu Rais Kikwete aliahidi wakulima wa chai Lupembe kuwa akirejea madarakani atamrudisha mwekezaji kiwandani ili waendelee kuuza chai yao na pia na kuhakikisha kiwanda kinakuwa na ulinzi lakini hadi leo ahadi hiyo haijatekelezeka jambo linalodaiwa kuwa kikwazo cha kutotekelezeka ahadi hiyo ni Bw.Luhanjo kwa kuwa kiongozi wa waliovamia kiwanda ni shemeji yake.

Hivi karibuni Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lilimtuhumu Bw. Luhanjo kwa kumdhalilisha waziri Mkuu na kuingilia uhuru na madaraka ya Bunge hatua iliyopelekea Spika Bi.Anna Mkinda kuunda kamati teule ya wabunge watano kuchunguza hatua hiyo.


No comments:

Post a Comment