20 September 2011

Kesi MV Spice kusubiri tume ya rais

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

MAHAKAMA Kuu ya Zanzibar imeshindwa kuendelea na kesi ya washtakiwa wa ajali ya meli ya MV Spice Islanders baada ya kuundwa Tume ya Kunchunguza ajali
hiyo.

Kesi hiyo ambayo ilitajwa kwa Mrajisi wa Mahakama hiyo, Bw. George Joseph Kazi inawahusisha watuhumiwa wanne akiwemo nahodha wa meli hiyo, Bw. Said Kinyanyite ambaye bado hajakamatwa.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Nahodha Msaidizi, Abdallah Mohammed Ali (30), Afisa Usalama wa Abiria wa Bandari Yussuf Suleiman Jussa (47) na Afisa Usalama wa abiria kutoka Mamlaka ya Usafiri Haharini, Simai Nyange Simai (27).

Hatua ya mahakama hiyo ilichukuliwa baada ya wakili wa washtakiwa hao, Bw. Hamid Bwezeleni kuiomba mahakama hiyo kusitisha kesi hiyo ili kuepusha mgongano wa maamuzi wa mahakama na tume hiyo.

Alisema kwa kuwa serikali imefikia uamuzi wa kuunda tume ya uchunguzi, hivyo kesi hiyo isimamishwe kwa sababu wateja wake pia watahitajika katika uchunguzi wa tume hiyo.

Alisema iwapo mahakama itaendelea na kesi na kutoa maamuzi, baadae wateja wake wabainike hawahusiki baada ya tume kukamilisha uchunguzi wake, utakuwa mgongano mkubwa wa kisheria.

Aidha wakili huyo alionesha wasiwasi katika uteuzi wa baadhi ya wajumbe wa tume hiyo kwa madai wamo wengine wana migongano kimaslahi kati ya taasisi zitakazohusika na uchunguzi.

Kwa upande wake, Mwenedsha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Ramadhan Nassib alisema maombi ya upande wa utetezi hayana msingi wowote kwa sababu maamuzi ya mahakama ni ya mwisho na kutaka kesi hiyo iendelee kama kawaida.

Aidha alisema hawezi kuzungumzia suala la uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo kwa sababu ni jukumu ambalo lipo nje ya uwezo wake.

Baada ya kusikiliza pande mbili, washitakiwa hao walipewa dhamana baada ya Mrajisi kuunga mkono ombi la utetezi na kueleza yuko tayari kuwaachia kwa masharti ya  kuwa na wadhamini wawili na ahadi ya sh. milioni 10 kila mmoja.

Washitakiwa hao walisomewa shitaka lao kwa mara ya kwanza Septemba 16, mwaka huu na kurejeshwa rumande baada ya upande wa mashtaka kuomba wanyimwe dhamana kwa sababu za kiusalama hasa kwa kuzingatia waathirika wa ajali hiyo bado wana kinyongo.

Ilidaiwa kuwa Septemba 9, mwaka huu, mnamo majira ya saa 3:30 za usiku huko katika bandari ya Malindi, Zanzibar; washitakiwa hao wote kwa pamoja waliruhusu kuingiza abiria na mizigo zaidi ya uwezo wa mali hiyo na kusababisha kuzama katika mkondo wa Nungwi majira ya saa 8:00 usiku, na hivyo kuu watu 203.

Msaada wa Barrick

Wakati huo huo Kampuni ya ya Afrika Barrick Gold imetoa sh. milioni 60 kusaidia waathirika wa ajali hiyo.

Msada huo ulikabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Balozi Juma Mwapachu katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi jana mjini Zanzibar.

Balozi Mwapachu alisema kwamba kampuni yao imeguswa na imeamua kutoa kiwango hicho cha fedha kama mkono wa pole kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake.

Meli ya MV Spice Islanders ilizama Septemba 10 mwaka huu, na kuuwa watu 204 na watu 619 waliokolewa wakiwa hai.

1 comment:

  1. Tatizo la Znz ni kuna kulindana sana na watu hupewa vyeo ili kulipa fadhila matokeo yake wanafanya kazi kwa mazoea tu! mwaka wa 20 huu mtoto wa jumbe in mkurugenzi wa bandari, haguswi, chombo cha ngapi hiki kinazama yeye yupo tu sijui ana direct nini! ma-agent wauza ticket kila pahala, kuanzia marikiti darajani, madukani, barabarani ili muradi tu tafrani kila mwenye kupata kiti na mwamvuli basi anauza ticket matokeo yake hakuna control ya kujua idadi ya abiria wakati wakurugenzi wapo, viongozi wote wapo, wanaona kinachoendelea na kukaa kimya! Na hata hao abiria mtu akikosa nafasi basi atampigia simu mkubwa yoyote ili naye apate safari, ndio mazingira ya kujuana na kulindana yalivyo, sijui hiyo timu itafanya miujiza ipi na tuone!

    ReplyDelete