15 September 2011

Igunga sasa ni ahadi kwa kwenda mbele

*Mgombea CUF,Lipumba waahidi neema

Na Peter Mwenda, Igunga

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Igunga kwa tiketi ya CUF, Bw. Leopold Mahona, amesema akichaguliwa atahakikisha ng’ombe na mbuzi wa
eneo hilo wanauzwa kwa kupima kwa kilo na atarejesha kiwanda cha ngozi.

Akihotubia mkutano wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, Bw. Mahona ambaye alifuatana na Mwenyekiti wa CUF,Profesa Ibrahim
Lipumba, alisema atafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo wanapata soko la kuuza pamba kwa bei nzuri na uhakika.

Katika kampeni hizo zilizoanza baada ya kuzilinduliwa juzi la Mwenyekiti wa CUF,Bw.
Lipumba, wananchi wa jimbo hilo pia wameahidiwa kujengewa chuo cha ufundi kwa ajili ya vijana wanaomaliza elimu yao ya msingi na Sekondari.

Akimnadi mgombea huyo, Profesa Lipumba ambaye alifanya mikutano mitatu katika kata
za Igurubi,  Choma na kumaliza mkutano wake wa mwisho katika Kata ya Nkinga alisema wananchi wa jimbo hilo wataondokana na matatizo lukuki kwa kumchagua Bw. Mahona.

Prof. Lipumba alisema wananchi wa Jimbo la Igunga wataendelea kuwa hoi kimaisha endapo hawatafanya mabadiliko ya kubadilisha uongozi wa CCM na kuweka uongozi mwingine wa CUF ambao utabadilisha maisha yao.

Alisema Igunga ni jimbo lenye utajiri mkubwa wa madini, kilimo cha pamba, ufugaji wa ng’ombe na rasilimali nyingine lakini wananchi wake wengi wanashindia mlo mmoja kwa siku kwa sababu hakuna viongozi wa kuhakikisha rasilimali zao zinatumika kwa manufaa yao wenyewe.

Profesa Lipumba alisema CCM imeshindwa kuleta mabadiliko kwa wananchi wake, hivyo ili jimbo la Igunga lianze kupata mafanikio kwa ajili ya vizazi vyao, ni lazima wakubali mabadiliko.

Alisema wakati akitoka Ulaya wiki iliyopita ndege aliyokuwa akisafiria ilishindwa kutua uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam kwa sababu ya taa kuzimika kutokana mgawo unaondelea nchini na kulazimika kurudi Nairobi ambako abiria
walitafutiwa ndege nyingine.

Alisema mgawo wa umeme ni mfano wa hali ngumu iliyoletwa na CCM ambayo iko madarakani kwa miaka 50 sasa huku wananchi wake wakiendelea kuishi maisha ya kubahatisha.

Alisema vyanzo vya upatikanaji maji ni vingi katika jimbo la Igunga, lakini hakuna mikakati ya kuna maji na kuchimba mabwawa ya kuhifadhia maji ambayo yatatumika wakati wa kiangazi kwa ajili ya kunyeshea mifugo na kilimo cha umwagiliaji.

1 comment:

  1. Wananchi wa Igunga wasingeweza kuwa na maendeleo kwa sababu Mbunge wao Rostam alijikita kwenye Ujangiri na Ufisadi. Hakuwa na mda kwa jimbo lake kwa sababu alijiaminisha kwa bosi wake JK ambao wamekuwa wakikufuru pamoja.

    ReplyDelete