29 September 2011

Dowans yaibwaga TANESCO

*Mahakama Kuu yaamuru ilipwe bil. 94/-

Na Rehema Mohamed

HATIMAYE Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imesajili tuzo ya sh. bilioni 94 ya Kampuni ya Kufua umeme ya
Dowans ambayo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lilikuwa likipinga isisajiliwe.

Uamuzi huo ulitolewa Dar es Salaam jana Jaji Emilian Mushi wa mahakama hiyo wakati akitoa uamuzi wa kisheria katika kesi iliyofunguliwa na TANESCO ya kupinga tuzo hiyo kusajiliwa.

Jaji Mushi alisema pamoja na kusajiliwa kwa tuzo hiyo, TANESCO imeamriwa kulipa gharama za uendeshaji kesi hiyo tangu ilipoanza. Hata hivyo gharama za kesi hiyo bado haijafanyiwa tathimini.

Uamuzi huo uliosomwa kwa saa tatu, utailazimu TANESCO kuilipa Dowans sh. bilioni 94.

Akitoa uamuzi wa kesi hiyo, Jaji Mushi alisema tuzo hiyo imesajiliwa kutokana na makubaliano ambayo TANESCO iliingia na Dowans katika mkataba wa pande hizo mbili.

Mojawapo ya makubaliano hayo ilikuwa kwamba uamuzi utakaotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) ndiyo utakuwa wa mwisho.

Alisema makubaliano mengine ni kwamba pamoja na ICC kuwa na uamuzi wa mwisho, hakutakuwa na ukataji wa rufaa kama upande mmoja utashindwa.

Pamoja na hilo, Dowans na Tanesco walikubalina kuwa mmoja kati yao atakayeshinda kesi ya tuzo hiyo, atalazimika kumlipa mwenzake mara moja.

Alisema kutokana na makubaliano hayo,mahakama ya ICC ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo, hivyo mahakama kuu haina mamlaka ya kutoa maamuzi mengine.

Hata hivyo, Jaji Mushi alisema upande ulioshindwa una haki ya kuiomba mahakama iweke tuzo hiyo kando kama wameona kulikuwa na makosa ya kisheria.

Uamuzi huo umeipa nguvu ya kisheria Dowans kulipwa fedha hizo kutokana na kuvunjwa kwa mkataba baina yake na TANESCO kinyume cha sheria.

Mmoja wa mawakili waliokuwa wakiiwakilisha TANESCO, Bi.Hawa Sinari alisema wanakwenda kufanya mashauriano na mteja wake ili waweze kukata rufaa.

Bi. Sinari alisema kabla ya kufanya hivyo kwanza wataupitia upya uamuzi wa  mahakama hiyo kabla ya kuchukua hatua zaidi.

"Kuna mambo mengi ya kukata rufaa, tunakwenda kufanya mashauriano na TANESCO baada ya kusoma upya uamuzi uliotolewa leo, ili tuweze kukata rufaa," alisema Bi. Sinari

Novemba 15, mwaka jana ICC chini ya mwenyekiti wake, Bw. Gerald Aksen na wasuluhishi Bw. Swithin Munyantwali na Bw. Jonathan Parker, iliiamuru TANESCO iilipe Dowans fidia ya sh. 94 bilioni kwa kuvunja mkataba kinyume cha sheria.

Januari 19, mwaka huu Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kiliwasilisha barua mahakamani kuu ikielezea nia ya kupinga usajili wa tuzo hiyo ili isisajiliwe.

Januari 25, Dowans kupitia wakili wake Bw. Kennedy Fungamtama iliwakilisha mahakamani hapo maombi ya usajili wa tuzo hiyo ili utaratibu wa ulipwaji wa fidia hiyo uwe na nguvu ya kisheria.

Baada ya Dowans kuwasilisha mahakamani hapo maombi hayo ya usajili, ndipo Januari 31, LHRC kwa pamoja na Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT) na Kampuni ya Sikika walipowasilisha rasmi mahakamani hapo pingamizi la usajili wa tuzo hiyo.

Tanesco nayo kwa upande wake, kupitia kwa wakili wake Rex Attorneys kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Februali 9, mwaka huu waliwasilisha mahakamani hapo pingamizi la usajili wa tuzo hiyo.

Septemba 6 mwaka huu Mahakama Kuu iliwaengua wanaharakati hao baada ya kutupilia mbali pingamizi lao.

1 comment:

  1. Na bado, huu ni mwamzo tu, tutafir...fir.. sote na mafisadi, dizaini kama popobawa vile

    ReplyDelete