*Timbe kutua leo
Na Zahoro Mlanzi
LICHA ya kutoa wachezaji wengi katika kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars', Klabu za Yanga na Simba zimesema hazina muda wa kupoteza
zinaendelea kujifua kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu Bara.
Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo ina wachezaji wanne ambao ni kipa Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Juma Seif 'Kijiko' na Nurdin Bakari na Simba wana Juma Nyosso, Juma Kaseja, Amir Maftah, Victor Costa na Salum Machaku.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Maofisa Habari wa klabu hizo, Louis Sendeu (Yanga) na Ezekiel Kamwaga (Simba) walisema mazoezi yanaendelea kawa kawaida baada ya kuwapa mapumziko ya siku mbili.
Kwa upande wa Sendeu alisema wao walianza tangu juzi katika uwanja wao wa Kaunda na kwamba kikosi chao kinazidi kuimarika baada ya waliokuwa majeruhi kuanza mazoezi.
"Mwape, Berko, Asamoah na Kigi wameanza rasmi mazoezi jana (juzi) chini ya Kocha Msaidizi, Felix Minziro na tunataka sasa hivi kuwapa raha mashabiki wetu katika michezo inayokuja baada ya kuanza vibaya michezo miwili iliyopita," alisema Sendeu.
Alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe atatua nchini akitokea kwao Uganda alipokwenda kupumzika pamoja na kuiangalia familia yake.
Alisema wachezaji wao wengine, Haruna Niyonzima na Hamis Kiiza wamekwenda kuyatumikia mataifa yao na kufanya kuwepo na pengo la wachezaji sita.
Naye Kamwaga alisema wataanza mazoezi leo kati ya viwanja vya TCC Sigara au Tanganyika Packers kwaniitategemea na Kocha Mkuu, Moses Basena atakavyopendekeza.
Alitamba kwamba kwa sasa timu yao ndio bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kutoa wachezaji wengi kuzitumikia timu za taifa kwani wametoa wachezaji tisa.
Wachezaji hao mbali na waliopo Stars ni Gervais Kago (Afrika ya Kati), Emmanuel Okwi (Uganda) na Jerry Santo (Kenya) ambapo wameitwa kwa ajili ya michezo ya kuwania kufuzu Mataifa ya Afrika.
No comments:
Post a Comment