23 August 2011

Upatikanaji wa maji waongezeka kwa 84%

Na Godfrey Ismaely

SERIKALI imesema upatikanaji wa maji safi katika mikoa 19 hapa nchini hususan miji mikuu umeongezeka kutoka asilimia 84 mwaka 2010 hadi asilimia 86 mwaka huu.Akiwasilisha
hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2011 na 2012,Mjini Dodoma jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Bw. Stephen Wassira kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo Profesa Mark Mwandosya alisema upatikanaji huo wa maji unaendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka.

Bw. Wassira alisema hali ya upatikanaji wa maji Dar es Salaam na miji ya Kibaha na Bagamoyo inayohudumiwa na DAWASA kwa sasa ni asilimia 55 kwa wastani wa saa 9 kwa siku ingawa bado kuna changamoto kubwa kutokana na ongezeko kubwa la watu mwaka hadi mwaka.

"Mheshimiwa mwenyekiti, Dar es Salaam, Kibaha na Bagamoyo miji inayohudumiwa na inayohudumiwa na DAWASA inakabiliwa na uhaba mkubwa wa huduma ya majisafi na huduma duni ya uondoaji wa majitaka," alisema Bw. Wassira

Waziri huyo alisema sababu zinazochangia uhaba wa maji ni pamoja na uchakavu wa miundombinu iliyopo ya kuzalisha na kusambaza maji, uondoaji wa majitaka ikiwamo kupungua kwa maji ya Mto Ruvu kutokana na uharibifu wa mazingira na ongezeko la vipindi vya ukame.

"Pia uwekezaji mdogo katika kuboresha na kupanua miundombinu ya kuzalisha na
kusambaza maji sambamba na ongezeko kubwa la idadi ya watu katika Jiji la Dar es Salaam la asilimia 6 kwa mwaka ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.5 katika mji mingine kitaifa," alisema Bw. Wassira.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo serikali imeandaa mpango wa kuboresha huduma ya maji safi na uondoaji wa majitaka Dar es Salaam unaolenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 300,000 kwa sasa hadi 710,000 kwa siku ifikapo mwaka 2014.

"Serikali ipo kwenye harakati za upatikanaji wa maji safi kutoka asilimia 55 za sasa hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2014, na kufikia asilimia 90 mwaka 2015 na kuongeza uwezo wa uondoshaji wa maji taka kutoka asilimia 10 za sasa hadi asilimia 25 ifikapo mwaka 2014," alisema Bw. Wassira.

Bw. Wassira alisema mpango huo ulianza kutekelezwa rasmi kuanzia mwezi Februari 2011 na umepangwa kukamilika mwaka 2013 na 2014.

"Mpango huo umekadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 653.85 ambapo kiwango hicho kitachangiwa na Serikali, Mfuko wa Pamoja wa Maji, Shirika la Marekani (MCC), Serikali ya Norway, na Serikali ya India," alisema Bw. Wassira.

Hata hivyo wizara hiyo imeliomba Bunge liidhinishe kiasi cha zaidi ya sh. bilioni 446 ili ziweze kutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo.




No comments:

Post a Comment