03 August 2011

Hatimaye bei ya mafuta yashuka

Na Rachel Balama

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)  imetangaza kushusha bei ya mafuta ya jumla na rejareja ikilinganishwa na ilivyokuwa katika toleo la Julai Mosi, mwaka huu.


Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, Bw. Haruna Masebu ilisema punguzo la bei kwa lita ya petroli ni sh. 202.37 sawa na asilimia 9.17, dizeli sh. 173.49 sawa na 8.32% na mafuta ya taa ni sh. 181.37 sawa na 8.70%.

Mlinganisho wa bei ya mafuta za Julai na zile za Agosti Mosi mwaka huu kwenye mabano ni sh.2,206.16 (sh.2,003.79); sh. 2,084.33 (sh. 1,910.84) na sh.2,085.90 (sh.1,904.53).

Alisema merekebisho yamefanywa kwenye tozo zinazokusanywa na taasisi mbalimbali za serikali kulingana na majukumu waliyonayo kwenye mfumo wa biashara ya mafuta.

Kwa mujibu wa Bw. Masebu, katika petroli imepunguzwa kutoka sh. 54.03 kwa lita hadi sh. 27.27 (49.53%); dizeli kutoka sh. 55.00 hadi sh. 28.15 kwa lita (48.80%) na kwa mafuta ya taa kutoka sh. 55.66 kwa lita hadi sh. 24.50 sawa na asilimia 55.98 kwa lita. Kwa ujumla, tozo za taasisi zimepungua kwa asilimia 51.44.

Alisema kwamba bei zingeshuka zaidi lakini kupanda kwa bei katika soko la dunia na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani, ambayo hutumika katika manunuzi ya bidhaa za mafuta kwenye soko la dunia.

Alizitaja changamoto zinazosababisha bei za mnafuta kuwa juu ni kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuyumba kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani kutaendelea kuathiri mwenendo wa bei za mafuta hapa nchini.

Alitolea mfano-Juni, mwaka huu thamani ya sarafu ya Tanzania ilikuwa ni sh. 1,555.31 ukilinganisha na dola; lakini sasa ni sh. 1,570.87.

3 comments:

  1. Hizo Tsh 200 mlizo ibia watanzania tangu kikwete arudi madarakani mwaka jana hadi leo, mnaweza kusema zimekwenda wapi? Sh 200 mara Idadi ya watanzania ambao ni mil zaidi ya 60 mara siku zote tangu Dec 2010 hadi leo ni Tsh ngapi? Waizi wakubwa nyie EWURA! Kwani hamkuona mfumuko wa bei ya mafuta tangu mwanzo?Leo mnajifanya eti kutokana na (merekebisho yamefanywa kwenye tozo zinazokusanywa na taasisi mbalimbali za serikali kulingana na majukumu waliyonayo kwenye mfumo wa biashara ya mafuta)
    Nanyi siku yenu yaja!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. Nchi hii sasa hivi ni kama haina serikali, Hata mafuta ya taa wanashindwa kuthibiti,Angalia bei ya sola ambazo serikali ilisema hazitozwi kodi, ni afadhali ukanunue Kenya ambako wanatoza kodi-Wizi gani huu. Hakika kuna siku Mungu atashusha gharika kutuangamiza wote. Madini yanatusaidia nini kama bado tuna matatizo makubwa kama haya. Maisha yamekuwa magumu sana kila kukicha. Serikali ya Kikwete imeshindwa na Inatakiwa wajiuzulu wote. Tumechoka!!

    ReplyDelete
  3. Mabilioni ya kikwete yamemnufaisha nani?, Ona sasa hivi tunatumia noti mbili tofauti zenye thamani sawa, hii ni kitu gani?, Hata ukienda benki ATM au counter utapewa noti ya zamani na mpya. Maajabu!!!! Huu sio wizi? Angalia Mshahara anaolipwa msomi aliyehitimu chuo kikuu(TGSD), hata kula tu haitoshi, Elimu haina thamani kabisa tanzania. Pesa zilizoibwa BOT zilirudishwa zilifanya kazi gani mbona hatujasikia kwenye baugtet, Mabilioni ya Rada na Ndege Mbovu ya Rais Nani kahusika na amechukuliwa hatua gani? Utasikia tu maneno ya kisiasa kutoka kwa viongozi tuliowapa dhamana ya nchi....tubekabidhi TAKUKURU wanachunguza.....
    Ujinga mtupu!!!!!
    Hatuana imani na Serikaki!!!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete