Na Suleiman Abeid, Meatu
UTARATIBU wa watoto wa shule za msingi kutembea umbali mrefu kila siku kwenda na kurudi shuleni ni moja ya sababu inayochangia matokeo mabaya ya mitihani wa
darasa la saba.
Wakichangia hoja mbalimbali katika kikao cha baraza madiwani kilichofanyika hivi karibuni kuhusu wilaya hiyo kuendelea kuwa na matokeo mabaya katika mitihani wa darasa la saba ,walisema umbali unachangia matokeo hayo mabaya.
Madiwani hao walisema baadhi ya watoto hutembea kati ya kilomita 12 na 16 kila siku kwenda na kurudi shuleni hali ambayo husababisha washindwe kufuatilia masomo.
Walisema upo umuhimu kwa madiwani, jamii na wadau wengine wa elimu wilayani humo kuhamasishana ili kujengwa shule katika vijiji jirani.
“Mwenyekiti, mimi nafikiri watoto wa wilaya ya Meatu ukijumlisha umbali wanaotembea kila siku kwenda na kurudi shuleni kuanzia darasa la kwanza hadi la saba
ni sawa wanakuwa wametembea kutoka Tanzania hadi nchi ya Libya , watoto wetu wanatembea umbali mrefu sana," alisema na kuongeza;
“Na hii ni moja ya sababu kubwa inayochangia matokeo mabaya katika mitihani ya kumaliza darasa la saba kila mwaka, wilaya yetu inakuwa ya mwisho, ni kweli, si rahisi mtoto atembee kilomita nane asubuhi kwenda shuleni na jioni kilomita hizo hizo anaporudi nyumbani halafu utegemee awe na matokeo mazuri, hapana,”
“Ni vizuri sasa tukaweka juhudi zetu katika kuhamasishana pale ambapo kijiji hakina shule ya msingi basi pajengwe shule, shule za mbali ni tatizo, si rahisi hata kwa
wazazi kufuatilia kuona kama mtoto amekwenda shule au ameishia njiani kucheza," alisema Diwani wa Kata ya Sakasaka, Bw. Peter Ndekeja na kuongeza;
"Inabidi sisi wenyewe tuzinduke, maana elimu ndiyo urithi pekee usiodaiwa mahakamani kama inavyotokea kwenye urithi wa mali nyingine."
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Bw. Abiudi Saideya, alisema utatuzi wa tatizo la kushuka kwa kiwango cha elimu katika wilaya ya Meatu lipo mikononi mwa wakazi wenyewe wa wilaya hiyo.
Bw. Saideya alisema wilaya ya Meatu inahitaji mabadiliko makubwa katika suala zima la kuinua kiwango cha elimu ili kuondoka na tatizo kushika nafasi ya mwisho.
“Mabadiliko yanahitajika, ni sisi wenyewe ndiyo tunaweza kuleta mabadiliko katika uboreshaji wa elimu, tusitegemee watu kutoka nje, na wananchi peke yao hawana uwezo huo bila ya kuwepo ushirikiano na viongozi wao,” alisema na kuongeza;
“Mara nyingi tunawatupia mzigo walimu na maofisa wao, lakini ni muhimu sasa sisi wenyewe tukasimama kidete, wazazi na viongozi tuhakikishe tunaondoa tatizo la watoto
wetu kutembea umbali mrefu.
No comments:
Post a Comment