21 August 2011

Chuo kikuu kutoa malazi, chakula bure kwa wanawake

Peter Mwenda na Grace Ndossa

CHUO Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha St. Joseph kimetoa ofa ya kulipa huduma za malazi na chakula bure kwa wanafunzi wanawake ambao watajiunga na
chuo hicho kuanzia mwakani.

Akizungumza katika mahafali ya tatu ya Chuo hicho, Mwenyekiti wa Bodi Padre Arul Raj alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa na chuo hicho kutokana na wanafunzi wengi wanawake kushindwa kujiunga chuoni kwa sababu ya gharama kubwa.

"Kuanzia mwaka huu wanafunzi wa kike ambao watajiunga na chuo chetu watakuwa wanapewa malazi na chakula bure ili waweze kusoma kwa bidii na idadi yao kuongezeka na hiyo itatolewa kwa wanafunzi wa kwanza kujiunga na chuo," alisema Padre Arul Raj.

Pia alisema chuo hicho kitajenga mabweni ya wasichana ambayo yataweza kulaza wanafunzi 240 hadi 300 ili kuwajengea uwezo wa kielimu katika masomo ya sayansi na teknolojia.

Alisema wameweka mikakati ya kuwawezesha wasichana nchini kusoma kufikia elimu za juu katika fani ya sayansi na teknolojia ambayo imeonekana kuwa kikwazo kwa wanafunzi hao.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. William Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka wanafunzi wengi waliomaliza chuoni hapo wafikirie kujiajiri wenyewe katika shughuli mbalimbali na kutengeneza ajira zao ili waweze kujipatia kipato.

Alisema anaamini wahitimu hao wamesoma kwa nadharia na vitendo hivyo taifa linategemea kupata wataalamu wa kuhakikisha mikakati mbalimbali ikiwemo Kilimo kwanza inasonga mbele.

"Tunategemea ujuzi na utaalamu mlioupata chuoni hapa mtautumia kufanya kazi katika nyanja za afya, kazi za kijamii na kutengeneza mashine na matrekta kusaidia Kilimo Kwanza," alisema Rais Mstaafu Mkapa.

Alisema Tanzania ina mashamba makubwa ambayo yanasubiriwa kuendelezwa katika kazi ya kilimo hivyo aliwataka watumie elimu waliyopata kuzalisha mazao katika mashamba makubwa na madogo.

Rais Mstaafu Mkapa alishauri chuo hicho kuanzisha maktaba ya vitabu mbalimbali kama zilizopo Nairobi nchini Kenya na Kampala nchini Uganda ambako watavitumia katika kusoma, kuzalisha na kutangaza masoko.

"Rafiki yangu Mhadhiri wa Chuo cha Uandishi wa habari siku moja aliwauliza wanafunzi wake kuwa ni wangapi kati ya 20 wamesoma vitabu vya mwezi uliopita? hakupata hata mmoja, akauliza tena wangapi wamesoma vitabu vya miezi mitatu iliyopita hakupata hata mmoja, akauliza miezi sita iliyopita hakupata hata mmoja kwa hiyo na nyinyi msifanye hivyo, "alisema Bw.  Mkapa na kushangiliwa na wahitimu hao.

Alisema mfano huo unawaasa wahitimu hao wasiache kusoma vitabu walivyokuwa wanafundishiwa shuleni kwani hiyo inawasaidia kupanua uelewa wao na kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa urahisi.

Alisema wahitimu hao wajue kuwa taifa lipo katika mdahalo wa kubadilisha katiba kwa hiyo ujuzi wao unahitajika na kutumia nafasi hiyo kushiriki kikamilifu.

Awali wakati akitembelea chuo hicho Rais Mstaafu Mkapa alilisifu Shirika la Masista Wadogo wa Mtakatifu Mary Immaculata wa Kanisa Katoliki kujenga chuo hicho na kushauri waendelee kujenga vyuo vingine.



1 comment:

  1. Tunashukuru kwa hilo , vile vile tunaomba angalau hata wavulana wafikiriwe ktk kupewa motisha hasa wale wanofanya vizuri darasani, kama shule itashindwa kupata vigezo.

    ReplyDelete