21 August 2011

Ada mpya kwa watalii yakoroga wenye hoteli

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya wabunge kushinikiza wenye hoteli za kitalii kulipa viwango vipya vya ada kwa watalii wanaotembelea mbuga za wanyama nchini, wenye
hoteli hizo wamekuja juu wakisema ulipaji wa ada hivyo ghafla utavuruga biashara ya utalii na kuwafanya wasiaminiwe.

Wakati wa kuchangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Mazingira wiki hii, wabunge waliwataka wenye hoteli kulipa ada hiyo mpya la sivyo waachane na biashara hiyo huku wenye hoteli wakipendekeza kwanza kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Hifadhi za Wanyamapori Tanzania (TANAPA).

Kuanzia Agosti mwaka huu, serikali kwa kupitia TANAPA iliongezeka malipo ya ada ya watalii kwenye mbuga za wanyama na hifadhi za taifa kutoka dola za Marekani 10 hadi kufika dola za Marekani 60 huku wenye hoteli wakilalamika kuwa hatua hiyo ilichukuliwa bila kufikia makubaliano nao na kuwa inavuruga uamninifu na wateja wao.

Serikali inasema kuwa ilifikia uamuzi wa kupandisha ada hiyo baada ya kugundua kuwa tozo kwenye chumba kimoja kwenye hoteli zilizoko kwenye mbuga za wanyama ni kati ya dola za Marekani 500 hadi 1000 huku wenye hoteli wakisema hawakuhusishwa katika suala hilo.

Wanalalamika kuwa kupandisha ada hiyo katikaki ya msimu wa utalii kutawafanya waonekana siyo waaminifu kwa watalii ambao tayari baadhi yao wamekwishalipa kabla hawajaja na kwamba utasababisha mazingira mabaya ya kufanya biashara ya utalii kwa ushindani na ufanisi nchini.

Katika barua waliyomwandikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Julai 21 mwaka huu kupitia Muungano wa Wafanyabiashara za Kitaali nchini (TCT) wwanailalamikia TANAPA kwa kupandisha ada ya watalii ambayo ilikubaliwa na kupitishwa na Bodi ya TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Chama cha Wenye Hoteli Tanzania (HAT) na TCT mwaka 2009.

Barua hiyo iliyosainiwa na Katibu wa TCT, Bw. Richard Rugimbana inasema mbaya zaidi uamuzi wa kupandisha ada umekuja katikati ya msimu wa ujio wa watalii ambapo mikataba mingi kati ya wenye hoteli hizo na watalii imekwisharidhiwa tayari.

"Tulikwishakubaliana kwenye mkataba kuwa hakuna nyongeza ya ada itakayofanywa katikati ya msimu wa utalii," inasema sehemu ya barua hiyo ambayo pia nakala yake ilitumwa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii na kuongeza:

"Tunaomba ofisi yako iingilie kati mgogoro huu. Tumekwisha wasilisha suala hili kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, lakini hakuna hatua iliyokwishachukuliwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu huu ni mgogoro mkubwa unaotishia kuvuruga sekta ya utalii ikiwa hautatafutiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo na uwazi."















No comments:

Post a Comment