31 August 2011

Answar Sunna 'kama kawa'

Waumini wa Kiislamu wa Answar Sunna Jijini Mbeya wakitawanyika mara baada ya kumaliza Ibada ya Swala ya Idi el Fitr katika eneo la Kiwanja cha Ngoma Sokomatola jana. Waumini wengine wa dini hiyo wanaswali Idi leo.
Na Rashid Mkwinda, Mbeya

WAUMINI wa dini ya Kiislamu wa madhehebu ya Answar Sunna jijini Mbeya jana wameungana na waislamu wengine duniani katika ibada ya swala ya  Idd el Fitri ikiwa ni
kukamilika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hata hivyo waumini hao wametofautiana na waumini wengine wa dini hiyo wanaoswali Idd leo huku kukiwa na malumbano ya kutofautiana kwa siku hiyo baina ya waislamu ambao baadhi yao wakiulaumu uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu nchini BAKWATA kutotoa taarifa za kuonekana kwa mwezi. 

Wakizungumza mara baada ya swala ya Idd jijini Mbeya walisema kuwa waumini hao walisema kuwa kwa wakati uliopo wa utandawazi BAKWATA hawakupaswa kuficha ukweli wa kuandama kwa mwezi popote duniani kwa kuwa taarifa za kuonekana kwa mwezi zimekuwa zikisambaa kwa mudsa mfupi kwa uwazi.

Bw.Hassan Mwakaje mkazi wa jijini Mbeya alisema kuwa BAKWATA wamekuwa wakifanya ukiritimba wa taarifa za kuandama kwa mwezi kila mwaka hali ambayo inaonesha kuwa hawako pamoja na waislamu bali wako kwa ajili ya maslahi zao na serikali.

Alisema kuwa taarifa za kuandama kwa mwezi zimethibitika kupitia Redio ya Kiislamu, Redio Imaan ambayo imenukuu watu kutoka wilayani Masasi mkoani Mtwara na kuwa kinachofanyika ni kuufedhehesha uislamu na waislamu na kwamba hata hivyo hakuna swaumu inayokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya Idd.

''Leo waislamu wote duniani wanaswali Idd, baadhi yetu bado wako katika mfungo na
taarifa za kuonekana kwa mwezi zimetangazwa waziwazi, hii ni hujuma dhdi ya
Uislamu,''alisema Bw.Mwakaje.

Aidha katika ibada ya swala Idd Shekhe Rajab Zunda alisema kuwa waislamu wanatakiwa
kukaa pamoja kumaliza tofauti zao ambazo zinasababisha migongano isiyo na msingi
zaidi ya kuendeleza kuudidimiza uislamu na waislamu kwa ujumla.

Akinukuu baadhi ya aya za Koran na Hadith za Mtume Muhammad (SAW) Shekhe Zunda
alisema Mwenyezi Mungu ameufanya Uislamu kuwa ni mwepesi bali watu wanaweka uzito
kutokana na maslahi zao katika dunia.

Naye Ustadh Ibrahim Bombo alisema kuwa Mwezi wa Ramadhan uwe ni kinga ya waumini kutoendelea na madhambi na kuwa wale watakaoingia katika madhambi wanafuata nyendo za shetani ambaye katika mwezi mzima wa Ramadhani alikuwa hana nafasi ya kuwarubuni waumini.

Alisema mwezi wa Ramadhani ulikuwa ni kinga na  tiba ya maradhi na madhambi na kuwa mara baada ya kumalizika kwa mwezi huo waumini wamebaki wakiwa wasafi wasio na dhambi hata chembe hivyo jitihada zinatakiwa kwa waumini kuendelea kudumu katika ibada.


No comments:

Post a Comment