Na Zahoro Mlanzi
MSHAMBULIAJI mpya wa timu ya Simba, Felix Sunzu amesema ataanza kuonesha makali yake Agosti 13, mwaka huu katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao
wa jadi Yanga.
Mchezo huo ni kwa ajili ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo itaanza Agosti 20, mwaka huu.
Aliitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam kwa simu baada ya kuulizwa kuhusu mchezo huo, ikiwa ndio utakuwa mchezo wake wa kwanza wa kimashindano kuitumikia timu hiyo, alisema anajua ni mchezo wenye ushindani mkubwa lakini atahakikisha anacheza katika kiwango kizuri.
"Ndio najua ni mchezo mgumu, hii debt kama ilivyo kwa TP Mazembe na Lupopo FC, Al Merreikh na Al Hilal, hivyo mashabiki wa Simba watarajie kuona mambo mazuri kutoka kwangu," alisema Sunzu.
Alisema pamoja na mchezo huo kuwa na ushindani lakini si kipimo tosha kwake kuangalia uwezo wake kwani anahitaji michezo zaidi.
Alisema anatarajia kukaa nchini kwao kati ya siku nne mpaka tano kuweka mambo sawa na familia yake ambapo baada ya hapo ndipo atakaporejea nchini kufanya kazi moja ya kufunga mabao.
Awali kabla ya Sunzu kuzungumza hayo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alithibitisha mchezaji huyo alitakiwa kuondoka jana baada ya kumkatia tiketi na kwamba atakaa nchini humo kwa wiki moja.
"Ni kweli Sunzu ameruhusiwa na uongozi kwenda nyumbani kwao kuaga, hivyo alishakatiwa tiketi ya kuondoka leo (jana) na atakaa huko kwa wiki moja," alisema Kamwaga.
No comments:
Post a Comment