Na Amina Athumani
MABINGWA watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Tanzania Bara, JKT Mbweni wametwaa kwa mara ya pili mfululizo ubingwa huo kwa kuichapa Jeshi Stars mabao
31-24 katika fainali iliyopigwa juzi jijini Arusha.
Akizungumza kwa simu akiwa Arusha jana, Kocha wa timu ya Taifa ya netiboli 'Taifa Queens', Mary Protus alisema JKT Mbweni wamenyakua ubingwa huo ikiwa hawajafungwa hata mechi moja katika michuano hiyo iliyokuwa na upinzani mkubwa.
Alisema JKT Mbweni imeibuka mabingwa baada ya kuifunga Jeshi Stars mabao 31-24 mchezo ambao ulionekana mkali na wakusisimua kutokana na timu hizo kuwa na asili ya ushindani kila zinapokutana.
"Kwa kweli ilikuwa ni fainali ya kukata na shoka kutokana na timu hizi kuwa na upinzani mkubwa kila zinapokutana na mara nyingi zimekuwa zikikutana katika fainali,"alisema Protus.
Alisema kutokana na ushindi huo, JKT Mbweni wanatwaa kwa mara mfululizo na pia ni mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza la mchezo huo.
Michuano hiyo ilishirikisha timu 16 kutoka klabu mbalimbali ambapo kwa mwaka huu mashindano hayo yalifanyika katika viwanja vya Shekh Amri Abeid, Arusha na kusimamiwa na Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA).
No comments:
Post a Comment