Na Frank Balile
UONGOZI wa klabu ya Simba, umesema mpaka mchana jana, walikuwa hawana mazungumzo yoyote na mshambuliaji wao wa zamani Mnigeria, Orji Obina.Mshambuliaji huyo
alitua hivi karibuni nchini huku baadhi ya viongozi wakitaka asajiliwe katika kikosi chao.
Akizungumza jana mchana, Msemaji wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa, mpaka jana mchana, hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanywa kati ya viongozi na mchezaji huyo.
“Mpaka natoka ofisini, hakuna mazungumzo yaliyofanywa kati ya viongozi na mchezaji huyo,” alisema.
Obina aliwasili mwishoni mwa wiki, ikiwa ni siku chache tangu kutua kwa mshambuliaji Mzambia, Felix Sunzu.
Kamwaga alisema kuwa, uongozi wa klabu hiyo unajipanga kuhakikisha kikosi chao kinakuwa imara kuanzia Ngao ya Jamii mpaka Ligi Kuu Bara.
Mbali na Obinna, Kamwaga alisema suala la wachezaji waliopelekwa kwa mkopo katika klabu mbalimbali za Ligi Kuu, linashughulikia ikiwa pamoja na kuwapa barua.
Kamwaga aliwataja wachezaji waliopelekwa kwa mkopo na timu wanazokwenda kwenye mabano ni Mussa Hassan 'Mgosi', Haruna Shamte na Mohamed Banka (Villa Squad).
Wengine ni Salum Aziz Gila (Coastal Union), Mohamed Kijusho, Meshack Abel (Ruvu Shooting) na Juma Jabu (Moro United).
Hata hivyo, baadhi ya wachezaji hao wamepinga kupelekwa kwa mkopo katika klabu hizo bila ya kushirikishwa.
Awali, habari zilizozagaa zilidai kuwa, mshambuliaji huyo angeweza kusajiliwa kama beki Mganda Derreck Walulya angetemwa, kitu ambacho ni kigumu kwani ni kipenzi cha benchi la ufundi na mashabiki wa klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment