19 July 2011

CHANEZA yasaka sh. milioni 2.5

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

CHAMA cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA), kinahitaji sh. milioni 2.5 ili kuweza kufanikisha zawadi za fedha taslimu kwa washindi katika Ligi Kuu ya Zanzibar ya
mchezo huo.

Akizungumza na gazeti hili,  Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho,  Rahima Bakari, alisema kiasi hicho cha fedha kama kitapatikana, kitasaidia kwa kiasi kikubwa katika ligi hiyo.


Alisema kama watapata fedha hizo,  wamepanga bingwa kumkabidhi sh. 500,000 na mshindi wa pili sh. 300,000, wakati mshindi wa tatu atapata sh. 200,000.

Hata hivyo, alisema wakati ligi hiyo ikiendelea, watajaribu kuomba  fedha hizo sehemu zitakazosaidia kuwapa washindi.

“Mpaka sasa hatujapata mfadhili, wala hizo pesa, lakini tunaendelea kutafuta kiasi hicho cha fedha ili kitusaidie,” alisema.

Ligi Kuu ya Zanzibar ya Netiboli inafanyika kisiwani Pemba, ikishirikisha timu 12,  sita za wanaume na sita za wanawake.

Alisema timu nne zinatoka kisiwani Pemba, wakati nyingine zinatoka Unguja.


Alizitaja timu zinazoshiriki ligi hiyo kwa upande wa wanawake kutoka  Unguja ni JKU, Ikulu, Zimamoto na Valantia, wakati kutoka Pemba ni Wete Stars na Chake Star.

Kwa timu za wanaume ni Polisi, JKU, Msambeni na Sogea zote kutoka Unguja, na Pemba ni Chake Boys na Wete Boys.

No comments:

Post a Comment