18 July 2011

Serikali yaokoa bilioni 217/-

Na Yusuph Katimba,Mtwara

2008/09-2010/11

SERIKALI mkoani Mtwara imeokoa sh. bilioni 217.22 kupitia kilimo cha korosho kwa msimu minne mfululizo kati ya 2007/2008 baada ya kuanzishwa kwa mfumo mpya wa Stakabadhi Ghalani.

Akizungumza na gazeti hili Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Anatori Tarimo , alisema Mkoa wa Mtwara umefanikiwa kuokoa kiasi hicho cha fedha kutokana na wananchi hasa wakulima wa zao hilo kuachana na mfumo wa zamani wa kuruhusu wafanyabiashara wadogowadogo (kangomba) kununua zao hilo kutoka kwa wakulima moja kwa moja.

Alisema mwaka 2007 wakati alipoanza kazi katika mkoa huo, alikuta utaratibu huo mbovu, ambapo wakulima pamoja na kuzalisha kiasi kidogo cha zao hilo, bado
wafanyabiashara hao walitumia mwanya huo kuwakandamiza kiasi cha kuona zao hilo halina mafufaa.

"Wakati naanza kazi katika mkoa huu, wakulima walikuwa hawanufaiki kabisa na zao hili, walikuwa wakilanguliwa, hata nilipoanzisha mfumo huu bado ulipata upinzani mkubwa kutoka kwa wale waliokuwa wakinufaika kwa mfumo huo," alisema Bw. Tarimo.

Alisema mfumo huo ulibadilisha maisha ya wakulima ambapo awali wakati ukianza kazi mkulima alikuwa akiuza korosho zake kwa wafanyabiashara wadogo kwa kiasi cha sh. 300 kwa kilo.

Alisema wakati mwingine wafanyabiashara hao walikuwa
wakilazimishwa kushusha bei zaidi hadi sh. 150.

Alisema hali hiyo ndiyo iliyomlazimisha kutafuta namna ya kukabiliana na wafanyabiashara hao kwa kuanzishwa mfumo mpya hivyo walianza kuuza korosho kwa 610  badala ya sh.300, ambapo tani 62,206 zilivunwa na
kupatokana  sh. bilioni 45.6

Alisema fedha hizo zilitokana na kuanzishwa kwa mfumo huo. Alisema kama korosho hizo zingeuzwa kwa mfumo wa zamani zingepatika sh. bilioni 18.66. "Mfumo huo  ulisaidia kuokoa sh. bilioni 26.94 kwa msimu huo,"alisema.

"Wakati naanzisha mfumo huu wale waliokuwa wakiwalangua wakulima walianza kupata hofu kutokana na mfumo huo, wale waliokuwa wakinufaika na mfumo huo wengine waliamua kuacha kazi na bado kuna wengine kwa sasa wameamua kukaa kimya," alisema.

Alisema, katika msimu wa 2008/09 wakulima wa korosho Mtwara walivuna tani 50,387 ambapo walipata sh. bilioni 47.28 na kila kilo ya korosho iliuzwa kwa sh.
675 badala ya sh. 300.

Alisema kwa msimu wa korosho wa mwaka 2009/10  jumla ya tani 49.806 zilivunwa, ambapo sh. bilioni 60.01 zilipatikana.

Alisema kama korosho hiyo ingeuzwa kwa bei ya zamani wangepata sh. 14.94,  kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani waliokoa sh. bilioni 45.07 msimu huo.

Alisema katika simu wa 2010/11 Mkoa wa Mtwara ulivuna tani 89,058, ambapo walipata sh. bilioni 136.85 kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani na kwamba kwa bei ta zamani wakulima wangepata sh. bilioni 25.81.

Kwa msingi huo alisema mfumo huo mpya uliweza  kuokoa sh. bilioni 111.04 na kwamba, kuanzia msimu wa kilimo cha korosho mwaka 2007/08-2010/11 Mkoa wa Mtwara ulifanikiwa kuokoa zaidi ya sh. bilioni
200.

Alisema kuwa,  Watazania wana moyo wa kujituma, kilichokosekana ni wasimamiaji walio na nia ya dhati katika kuendeleza na kuboresha maisha ya wakulima
nchi.

No comments:

Post a Comment