Na Addolph Bruno
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya nchi, imetoa onyo kwa wanamichezo na raia wa kigeni wanaoingia nchini kwa shughuli za michezo kuacha kutumia fursa ya michezo na
kuingia katika masuala ya ukimbizi.
Kauli hiyo imetolewa siku chache, baada ya wachezaji 13 wa timu ya Red Sea ya Eritrea waliokuwa wakishiriki michuano ya Kombe la Kagame, iliyomalizika hivi karibuni kushindwa kuondoka nchini.
Timu hiyo ambayo ilitolewa katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, ilitarajiwa kurejea kwao Julai 9 mwaka huu lakini walishindwa kusafiri na kubaki nchini wakiomba hifadhi ya ukimbizi.
Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana, Msemaji wa wizara hiyo Isaac Nantanga, alisema serikali haiko tayari kuvumilia vitendo vinavyofanywa kinyume na taratibu hata kama michezo ni sehemu ya burudani.
"Malengo ya sasa ya serikali ni kuhakikisha kwamba hadi kufikia mwaka 2012, wakimbizi wote wamepelekwa kwao na kambi zote zinafungwa, kwa hiyo wanamichezo na raia wengine watambue hilo kwani serikali haitalifumbia macho hata kama ni masuala ya burudani," alisema.
Alisema kuhusu wachezaji hao wa Eritrea, serikali kupitia Idara ya Wakimbizi inayoshughulikia hifadhi watu, imefanya nao mahojiano na taarifa inaandaliwa kupelekwa kwa uongozi wa juu wa wizara ambao watachukua hatua.
"Baada ya kufanya mahojiano hatua nyingine inayofuata nayo ni kuandaliwa kwa taarifa itakayopelekwa kwa uongozi, ambao utatoa taarifa juu ya wachezaji hao," alisema Nantanga.
Alisema wachezaji hao kwa sasa bado wanashikiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), mpaka Wizara itakapolitolea uamuzi suala hilo.
No comments:
Post a Comment