Na Amina Athumani
SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) lipo kwenye mazungumzo na serikali kuhusu kuwasaidia kuanzisha kituo cha kuibua vipaji vya mchezo huo cha
'Tanzania Basketball Academy'.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TBF, Alexander Msofe alisema mchakato huo tayari umeanza na watashirikiana na serikali ili kuona ni jinsi gani wataweza kusaidiana katika suala hilo.
"Kupitia mashindano haya ya Umoja wa Shule za Sekondari (UMISSETA), kuna vipaji vingi tumevipata na sisi kama TBF tumetuma jopo la viongozi wa mchezo huu Kibaha pamoja na mimi mwenyewe kwa ajili ya kufuatilia kwa makini tangu mashindano haya yaanze.
"Kutokana na programu yetu tuliyoiweka kwa muda mrefu ya kuwa na kituo cha michezo kama zilivyo nchi nyingine zilizoendelea katika mpira wa kikapu, tumeona ni vyema vipaji tulivyovipata kwenye UMISSETA vipatiwe njia mbadala ya kuviendeleza," alisema Msofe.
Msofe alisema kuwepo kwa kituo maalumu cha kuendeleza mpira wa kikapu nchini, kutasaidia kuibua wanamichezo wengi nyota watakaoweza kufanyiwa majaribio katika nchi mbalimbali kama ilivyotokea kwa mchezaji nyota wa Tanzania anayechezea ligi ya mpira wa kikapu nchini Marekani (NBA) Hasheem Thabeet.
No comments:
Post a Comment