22 June 2011

Malecela afanyiwa upasuaji wa moyo

Na Grace Michael, Dodoma

WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. John Malecela, amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo nchini India hatua iliyomfanya Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Bi. Anne Malecela, kutohudhuria
mkutano wanne wa Bunge la bajeti tangu uanze.

Taarifa hizo zilijulikana Bungeni mjini Dodoma jana wakati Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda akiwasisitizia wabunge kuhudhuria kikao cha jioni ili kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012.

“Waheshimiwa wabunge kila mmoja ahakikishe anahudhuria kikao cha jioni, Mawaziri wa Fedha wataanza kujibu hoja, muda wa kupitisha bajeti ukifika, kila mmoja atahojiwa na kujibu hivyo ni muhimu kila mmoja kuwepo,” alisema Bi. Makinda.

Pamoja na kuwataka wabunge wote na mawaziri kuwepo kikao cha jioni, Bi. Makinda alitoa taarifa ya kutoonekana kwa Naibu Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai ambaye alisema kuwa yuko nchini Uingereza pamoja na wabunge wengine watatu.

Alimtaja pia Bi. Malecela na akaeleza kuwa “Mzee Malecela amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo ndio maana hata mama Kilango haonekani,” alisema Bi. Makinda.

Bi. Makinda aliwasihi wabunge wote kuhakikisha wanahudhuria kikao hicho ili kukamilisha jukumu zito la kupitisha bajeti.

No comments:

Post a Comment