17 June 2011

Simba yatua Congo, yaanza kujifua

Na Zahoro Mlanzi

WAWAKILISHI waliobaki katika mashindano ya kimataifa, timu ya Simba imeondoka alfajiri ya jana kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kutua
nchini humo salama na kuanza mazoezi moja kwa moja.

Timu hiyo itaumana na DC Motema Pembe ya nchini humo, Jumapili katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho (CAF).

Katika mchezo wa awali uliopigwa wiki iliyopita Jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele ambapo katika mchezo huo wawakilishi hao wa Tanzania wanahitaji sare ya aina yoyote, ili iweze kufuzu.

Akizungumza kwa simu akiwa Jijini Kinshasa jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu' alisema timu yake imetua nchini humo salama na kulakiwa na mashabiki wa timu hiyo waliopo huko.

"Tuna mshukuru Mungu tumefika salama na kwamba tumepokewa vizuri na Watanzania wanaoishi huku na tunapumzika kwa muda lakini, baadaye jioni tutafanya mazoezi ya kujiwinda na mchezo huo," alisema Kaburu.

Alisema waliamua kwenda mapema nchini humo ili kupata muda mzuri wa kuzoea hali ya hewa ya huko, pamoja na kuweka sawa mambo mengine ya msingi.

Akizungumzia suala la minong'ono iliyoenea Dar es Salaam kuhusu kusogezwa mbele kwa mchezo huo, alisema yeye hajui kwa kuwa ilisambazwa hivyo lakini cha kushangaza walipofika hali ilikuwa tofauti.

"Zile taarifa zilizodaiwa kutolewa na CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika) nadhani hazikuwa sahihi maana huku kuna shamrashara za huo mchezo kila kona," alisema Kaburu.

Endapo Simba ikifanikiwa kutinga hatua ya makundi itakutana na timu za Sunshine ya Nigeria, Maghreb de Fes ya Tunisia na JS Kabylie ya Morocco zilizopangwa Kundi B.

No comments:

Post a Comment