Na John Gagarini, Kibaha
TIMU ya soka Kanda ya Dar es Salaam imeipeleka mchaka mchaka timu ya Kanda ya Ziwa na kuicharaza mabao 3-0 kwenye mchezo wa michuano ya
Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA), taifa inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kuvutia ulikuwa na ushindani mkubwa lakini Dar es Salaam, waliweza kuwabana wapinzani wao ambao walishindwa kufurukuta kabisa.
Kanda ya Dar es Salaam iliandika bao kwanza dakika ya 22 kupitia kwa Juma Gunda, ambapo Raidhan Hafidh aliiandikia timu yake bao la pili dakika ya 27.
Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ambayo hata hivyo yaliwasaidia zaidi Dar es Salaam.
Raidhan Hafidh kwa mara nyingine alifanikiwa kutikisa nyavu za Ziwa dakika ya 54 na kuwanyamazisha kabisa mashabiki wa Ziwa ambao walikuwa na imani kuwa timu yao ingeshinda mpambano huo.
Kwenye mchezo mwingine Kanda ya Zanzibar iliifunga Ziwa Magharibi mabao 2-0, huku Mashariki nao wakiendeleza dozi kwa kuichabanga Kaskazini Magharibi mabao 4-0.
Kwa upande wa soka la wanawake, Kanda ya Mashariki ilitoa kipigo kikali kwa Nyanda za Juu Kusini kwa kuichabanga mabao 7-0, huku upande wa netiboli Kanda ya Mashariki ikiendelea kutamba kwa kuichabanga Magharibi kwa mabao 18-4.
Kwenye mchezo wa mikono wasichana, Kanda ya Nyanda za Juu waliwafunga Kaskazini Magharibi kwa pointi 12-7, huku Ziwa wakiwafunga Kati kwa pointi 32-12, Kikapu wanawake Kaskazini Magharibi waliwashinda Kusini kwa vikapu 15-10 na Nyanda za Juu waliwafunga Magharibi kwa vikapu 25-20 wavulana.
Mchezo wa Voleyball wasichana Kaskazini Mashariki iliifunga Dar es Salaam kwa seti 3-0, mchezo mwingine wa kikapu wanaume Ziwa iliifunga Kaskazini Magharibi kwa vikapu 19-7, Nyanda za Juu ikaifunga Kaskazini Magharibi kwa vikapu 8-7 kwa upande wa wanawake, huku Ziwa wakiwafunga Kati kwa vikapu 32-13.
No comments:
Post a Comment