15 June 2011

Mchungaji Rwakatare kuhojiwa kwa kushindwa kutangaza mali

Na Agnes Mwaijega

MBUNGE wa Viti Maaluma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Dkt. Getrude Rwakatare, anatarajiwa kuhojiwa leo na Baraza la Maadili kutokana na
kushindwa kuwasilisha fomu ya tamko kwa tume ya maadili juu ya mali anazomiliki.

Kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizoainishwa na Tume ya maadili, kiongozi yeyote wa umma ni lazima ajaze fomu za matamko kila inapofika Desemba na kwamba kushindwa kufuata utaratibu huo kwa kiongozi yeyote ni kosa linalostahili hatua za kisheria.

Pamoja na kuitwa mbele ya baraza kueleza sababu za msingi za kushindwa kujaza fomu hizo na iwapo maelezo yake hayataridhisha, Mchungaji Rwakatare anaweza kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Jaji Damian Lubuva, alisema madhumuni ya kuwaita viongozi mbalimbali ambao wameshindwa kuwasilisha matamko ya mali wanazomiliki kwa wakati ni hatua muhimu katika kuhakikisha kila kiongozi wa umma anaheshimu na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na tume ya maadili ya viongozi wa umma.

Katika hatua nyingine Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, Bw. Silvatory Machemli, ambaye aliitwa jana na baraza hilo, alisema sababu za kushindwa kujaza fomu hizo kuwa ni pamoja na tume ya maadili ya viongozi wa umma kutokuwa na utaratibu mzuri wa kuhakikisha fomu hizo zinawafikia.

Alidai alishajaza fomu za matamko na kuzirejesha na kushangaa kuitwa tena kudaiwa.

"Nashangaa kuona naitwa mbele ya baraza kuulizwa fomu ziko wapi wakati nilishajaza na sijawahi kupata barua zilizotumwa na tume ya maadili kupitia kwa spika kunikumbusha kujaza fomu hizo kama sijajaza," alisema.

Alisema utaratibu unaotumiwa na tume ya maadili wa kumpa spika wa bunge barua za kuwakumbusha viongozi ambao hawajaza fomu siyo mzuri na hazikupaswa kupitia kwa kiongozi huyo, kwa kuwa hajui ambao hawajajaza fomu hizo kwa wakati, hivyo hutoa tangazo bila kusema nani anatakiwa kujaza.

"Utaratibu huu siyo mzuri na wala tume haipaswi kumtumia spika wakati mhusika yupo," alisema mbunge huyo.

Vyombo vya habari jana viliwataja wabunge wengine wanaotakiwa kuhojiwa kuwa ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe, Riziki Lulinda, Devotha Likokola, Felix Mkosamali na Kapteni John Komba.

2 comments:

  1. kama wabunge wanajaza fomu za maadili mbona hatujawahi kusikia mafisadi wanachukuliwa hatua ya kuwa na mali nyingi?

    ReplyDelete
  2. Yaani binada akipewa milima 2 ya dhahabu,atataka na wa 3 pia uwe wake. Tukumbuke kuwa kuna KUFA jamani! Tutaviacha tu.

    ReplyDelete