03 June 2011

Kamati yawatimua Kariakoo, NARCO kwa ubabaishaji

Na Grace Michael

KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) jana ililazimika kuyatimua mbele yake Shirika la Masoko Kariakoo na Ranchi ya Taifa (NARCO) baada ya
kubaini ubabaishaji katika uendeshaji wake.

Shirika la Masoko Kariakoo ndilo lilikuwa la kwanza kutimuliwa kutokana na bodi iliyofika mbele ya kamati hiyo kuwepo kwenye nafasi hizo za uongozi kinyume cha sheria.

Baada ya uongozi huo kujitambulisha mbele ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Zitto Kabwe alianza kumhoji Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Bw. Bakari Kingobi kama yupo kihalali au kwa mujibu wa sheria katika nafasi hiyo.

Bw. Kingobi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji, aliyeonekana kutambua wazi kuwa yupo isivyo halali, alikiri kuwa mpaka sasa anashika nafasi hiyo kinyume na sheria na akaweka wazi kuwa tayari ameandika Barua TAMISEMI akikumbusha umuhimu wa kuteuliwa kwa bodi mpya baada ya bodi hiyo kumaliza muda wake.

Suala jingine ambalo liliibuliwa ni namna Mwenyekiti huyo alivyoteuliwa kinyume cha sheria ambapo aliteuliwa na TAMISEMI badala ya kuteuliwa na Rais kama sheria inavyotaka.

Pamoja na wajumbe wa kamati hiyo kuhoji mambo mbalimbali yanayohusiana na upotevu wa mali za shirika hilo zikiwemo nyumba, viwanja na mali zingine lakini Bw. Zitto alilazimika kusitisha maswali na hayo na kuamua kuwatimua viongozi hao kwa kuwa hawakuwa halali mbele ya kamati hiyo.

"Nimepata ushauri wa kikanuni hapa, tumebaini kuwa watu tulionao mbele yetu si ambao tunawahitaji na tukiendelea kuwahoji na sisi tutavunja sheria, hivyo waondoke na kamati itawasiliana na TAMISEMI ili mchakato wa uteuzi wa bodi mpya ufanyike haraka," alisema Bw. Zitto na kuongeza;

"Kuna madudu mengi kwa kuwa uongozi wa shirika umezidiwa nguvu na wafanyabiashara, imefika mahali nyumba na hata viwanja vinachukuliwa tu na watu na kupotea bila sababu ya msingi, hivyo tutahakikisha tunalifanyia kazi suala hili," alisema.

Mbali na hilo, Bw. Zitto pia alisema kuwa kamati itaomba ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) baada ya kuagizwa na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ili kujadiliwa.

Kwa upande wa NARCO walijikuta wakifukuzwa baada ya kushindwa kuieleza kamati idadi ya ng'ombe waliopotea na waliokufa.

Wajumbe wa Kamati walihoji kuongezeka kwa takwimu za ng'ombe wanaokufa na kupotea katika ranchi mbalimbali, hatua iliyowafanya waombe ufafanuzi zaidi kutoka kwa viongozi hao.

Akijibu hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya NARCO, Bw. Salum Shamte, alisema kuwa kwa wakati huo hawakuwa na idadi sahihi lakini akatoa idadi ya ng'ombe 55 walioibwa katika ranchi ya Kongwa.

Alisema kuwa wizi uliofanyika Kongwa walibaini kuhusika kwa meneja wa ranchi hiyo ambapo walimchulia hatua ya kumwachisha kazi.

Akihoji hatua hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Ester Bulaya, alishangazwa na hatua ya kumwachisha kazi peke yake bila ya kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria ili hatua zaidi zichuliwe.

"Kwa nini huyu mtu aishie kufukuzwa kazi tu...? Haiwezekani, ni lazima hatua zaidi zichukuliwe kwani suala hilo mmelifuatilia kwa muda gani ili kujua polisi wamefikia wapi? alihoji Bi. Bulaya.

Hata hivyo Bw. Zitto aliagiza uongozi huo kuandika barua polisi ili kujua uchunguzi wa suala hilo umefikia wapi na majibu hayo yafikishwe mbele ya kamati kwa ufuatiliaji zaidi.

Bw. Zitto alisema kuwa anapata mashaka na idadi kubwa ya upotevu na vifo vya ng'ombe hivyo akautaka uongozi huo kuondoka ili ujiandae na takwimu zitakazoonesha idadi halisi ya ngombe waliokufa na kupotea.

"Haiwezekani idadi hiyo itoke asilimia 10 na kufikia asilimia 30, hii inaonesha kuna njama fulani hatutakubali...maeneo mengine mmefanya vizuri lakini hili hapana, kajipangeni upya," alisema Bw. Zitto.

No comments:

Post a Comment