03 June 2011

Mauaji Ngara viongozi wilaya lawamani

Na Theonestina Juma, Bukoba

MAUAJI ya kutisha ya Watanzania sita katika pori la Rubagabaga kijiji cha Murbaga kata na tarafa ya Mursagamba wilayani Ngara na wafugaji haramu wenye
asili ya Kinyarwanda yanadaiwa kutokana na baadhi ya viongozi wilayani humo kuwakingia kifua wafugaji haramu kwa ajili ya maslahi binafsi.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wananchi wa wilayani humo, wakati wakizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kwa sharti la kutotaka kutajwa majina yao.

Wananchi hao walisema kwa kipindi kirefu wamekuwa katika wilaya hiyo wakulima na wafugaji haramu wamekuwa wakizozana lakini hakuna hatua ambayo inachukuliwa na viongozi husika zaidi ya mifugo ya wafugaji hao kuwaharibia mazao yao.

Mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Salum Nyakonji hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi kuzungumzia suala hilo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Bw. Vitus Mlolere suala hilo linafanyiwa uchunguzi ili kubaini ukweli wake licha ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa wapo viongozi wa wilaya ambao wamekuwa wakiwalinda wafugaji haramu hao.

Kamanda Mlolere alisema katika tukio hilo la Mei 30, mwaka huu kundi la wafugaji lilipambana na wakulima wa kijiji cha Murbaga ambapo chanzo kilikuwa ni kugombea pori hilo.

Kamanda Mlolere alisema Jeshi la polisi linamshikilia mfugaji moja mwenye asili ya Kinyarwanda kwa mahojiano zaidi lakini hakuwa tayari kutaja jina lake.

Waliouawa katika tukio hilo ni pamoja na Kabaranye Daniel chiza (70), Benedicto Bashogongo (65), Selestine Mawela (47) Damian Rusela (25), Nyivuyekula kasonga (48) na Sylvan us Benedicto (22).

No comments:

Post a Comment