03 June 2011

Henry Joseph, Chombo watemwa Stars

Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya taifa 'Taifa Stars', imeondoka alfajiri ya leo kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati huku ikiwaacha wachezaji wake Henry Joseph, Kigi Makasi na Ramadhan Chombo
'Redondo' kwa sababu mbalimbali.

Stars inatarajiwa kutua jijini Bangui nchini humo, tayari kwa mchezo wao utakaopigwa Jumapili wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.

Fainali hizo zinatarajiwa kufanyika katika nchi za Gabon na Guinea ya Ikweta ambapo mchezo huo na mwingine wa kundi lao la D, litatoa picha halisi ya watakaoongoza baada ya timu zote kuwiana kwa pointi nne.

Akizungumza muda mfupi baada ya timu kukabidhiwa bendera na Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Kipingu, Ofisa Habari Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema Henry ni mgonjwa hivyo hatosafiri na timu.

"Pia Makasi na Ramadhan Chombo nao hawatakwenda kwa kuwa kama mnavyojua wanatakiwa wachezaji 20 tu, hivyo hawa wameachwa kutokana na nafasi," alisema Wambura.

Aliwataja wachezaji wanaoondoka ni makipa Shaaban Kado na Shaaban Dihile, mabeki ni Shedrack Nsajigwa, Nadir Haroub 'Canavaro', Idrisa Rajab, Amir Maftah, Juma Nyoso na Aggrey Morris.

Wengine ni Mwinyi Kazimoto, Jabir Azizi, Nizar Khalfan, Nurdin Bakari, Shaaban Nditi, Mohamed Banka, Julius Mrope, Mrisho Ngassa, Mbwana Samatta, Athuman Machupa, John Bocco na Salum Machaku.

Kabla ya Wambura kuzungumza mgeni rasmi, Kipingu aliwataka wachezaji waelewe umuhimu wa mchezo huo kwani ndiyo utakaotoa mwelekeo wa timu ipi itakuwa katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Alisema lazima watambue mazingira ya huko si kama ya kwao kwani wapo ugenini, hivyo ni lazima wacheze kufa au kupona kuhakikisha wanashinda.

"Timu yetu sasa hivi hata ikifungwa watu hawacheki na hii kwa sababu wanapigana, naomba Watanzania waiombee kwa dua za aina yoyote," alisema Kipingu.

Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen alisema timu yake imejiandaa vizuri na kuyafanyia kazi yale makosa yalijitokeza katika michezo miwili waliyopoteza ya kirafiki ya kimataifa.

Alisema atahakikisha wachezaji wake wanacheza soka la uhakikia, ili kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa ugenini.

No comments:

Post a Comment